Wananchi 71,960, wa Tarafa ya M barika, Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza kuanza kunufaika na huduma za uzazi kwa akina mama wajawazito na watoto baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Wodi ya Wazazi Kituo cha Afya Mbarika.
Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki jana wakati wa hafla ya kukabidhi Jengo la Wodi ya Wazazi katika Kituo cha Afya Mbarika, Wilayani Misungwi lililojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Global Affair la nchini Canada kupitia Mradi wa Mama na mtoto uliokuwa unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na Halamshauri ya Wilaya ya Kwimba, Mkoani Mwanza kuanzia mwaka 2016.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mradi na hali ya utoaji wa huduma za Afya, katika Kituo cha Afya Mbarika iliyowasilishwa na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Mbarika, Dkt, Barnabas Makanza amesema kuwa Jengo la Wazazi limetekelezwa na kujengwa chini ya usimamizi wa Mhandisi wa Halmashauri kwa gharama ya shilingi Milioni 156 hadi kukamilika, ambapo Shirika la Global Affair la Canada lilitoa fedha shilingi Milioni 146, mchango wa Halmashauri wa shilingi Milioni 5 na jamii imechangia mawe, mchanga na nguvu kazi ya kuchimba msingi na maji ambao ni mchango wenye thamani ya shilingi Milioni 5.
Dkt, Makanza amesema kwamba Jengo hilo la Wodi ya Wazazi lina uwezo wa kuweka vitanda 31 vya kuhudumia Wazazi na uwezo wa kuhudumia Wazazi wanne kwa wakati mmoja pamoja na uwezo wa vitanda vinne vya kujifungulia (derivery beds), ambapo mradi huo pia umewezesha kujengwa kwa Jengo la Upasuaji ambalo lilikamilika kwa gharama ya shilingi Milioni 194 na tayari limeshaanza kutoa huduma kwa Wagonjwa wa upasuaji.
Akizungumza na Wananchi wa Tarafa ya Mbarika, Afisa Tawala Wilaya ya Misungwi, Zubeda Kimaro kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda, alieleza kwamba amekagua ujenzi wa Jengo hilo na kujiridhisha zaidi kwamba ujenzi umefanyika vizuri ambapo Jengo hilo limejengwa kwa kiwango na ubora, sambamba na kuwa na vyumba vya kutosha kuweka vitanda vya kuwahudumia akinamama wajawazito kwa wakati mmoja na kusisitiza kuwekwa kwa vitanda hivyo na vifaa tiba vingine ili huduma kwa Wazazi zianze kutolewa mapema, pia ameelekeza Jengo hilo liitwe “Tanya Maternity Ward “ kwa lengo la kutambua mchango wa Meneja mradi huo.
Bi, Zubeda Kimaro, amewataka Wananchi wa Tarafa ya Mbarika kuitumia kikamilifu na kuitunza Wodi hiyo ya Wazazi ili akinamama waweze kujifungua katika hali salama na bora ili kupunguza na kuondoa vifo vya akina mama Wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano, ambapo amewashukuru wawakilishi wa Shirika la Global Affair la nchini Canada ambalo limetekeleza Mradi huu wa Mama na Mtoto na kuwapongeza kwa juhudi na ufadhili waliutoa katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa kipindi chote.
Mganga Mkuu Wilaya ya Misungwi, Dkt, Zabron Masatu alifafanua na kueleza kwamba, Tarafa ya Mbarika Wilayani Misungwi ni moja kati ya maeneo yaliyokuwa yameshamiri na kuongoza kwenye Vifo vya akina mama na Watoto chini ya miaka mitano kutokana na adha ya kukosekana kwa huduma za uzazi kwa wananchi hao , hivyo kupitia uongozi wa Halmashauri waliamua kusogeza na kuongeza upatikanaji wa huduma ya Afya ya mama na mtoto kwa kujenga Jengo la upasuaji pamoja na Wodi ya Wazazi kupitia ufadhili wa Mradi wa Mama na mtoto.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa mama na mtoto, Tanya Salewski amesema kwamba Mradi wa mama na mtoto umetekeleza miradi ya kusaidia na kuimarisha huduma za uzazi kwa akina mama na watoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi tangu mwaka 2016, na wamefanikiwa kujenga Jengo la upasuaji, na sasa wamekamilisha ujenzi wa Wodi ya Wazazi na mwanzoni kabla ya kuanza mradi walitoa ufadhili wa gari la Wagonjwa (Ambulance) ambalo limeweza kutoa huduma katika Kituo cha Afya Mbarika, pamoja na ukarabati wa Jengo la Wagonjwa wa nje katika Zahanati ya Nyamayinza na ukarabati wa chumba cha upasuaji mdogo katika Zahanati ya Mwawile.
Meneja Mradi wa mama na mtoto, Tanya ameeleza kwamba tayari wameweka utaratibu wa kutoa vifaa tiba ambapo wiki ijayo wataleta vifaa tiba hivyo kwa ajili ya matumizi ya Wazazi kujifungulia, pia amewaomba Wananchi wa Mbarika kuvitumia vizuri na kuvitunza ili vidumu kwa muda mrefu zaidi pamoja na kuwashukuru kwa ushirikiano waliouonyesha katika mradi huo na kuwataka kuendelea na moyo huo wa upendo na ushirikiano.
Katika hafla hiyo ya makabidhiano Mradi wa Mama na mtoto wameweza kukabidhi na kutoa gari aina ya Toyati Nissan yenye namba za usajili T 796 DKG lenye thamani ya shilingi Milioni 140 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Meneja Mradi wa Mama na mtoto Bi,Tanya Salewski akimkabidhi funguo za Gari aina ya Toyata Nissan yenye namba za usajiri T 796 DKG, Afisa TawalaWilaya ya Misungwi, Bi, Zubeda Kimaro kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Misumgwi, Juma Sweda, Gari hilo limetolewa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ili kusaidia shughuli za utoaji wa huduma za afya kwa Wazazi na watoto chini ya miaka mitano.
Mratibu wa Mama na mtoto,Bi, Halima Bumbo (kushoto) akifuatiwa na Meneja Mradi wa Mama na mtoto Tanya Salewski wakati wa makabidhiano ya vifaa vya kusaidia watoto kupumua (baby woma ambavyo vimekabidhiwa na mradi huo wa mama na mtoto kwa Wilaya ya Misungwi.
Afisa Tawala Wilaya ya Misungwi, Bi, Zubeda Kimaro akizungumza na Viongozi na Wananchi wa Tarafa ya Mbarika kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda alipomwakilisha katika hafla ya Makabidhiano ya Jengo la Wodi ya Wazazi katikaKituo cha Afya Mbarika Jengo hilo lilijengwa kwa ufadhili wa Mradi wa Mama na mtoto kwa gharama ya shilingi milioni 146, (kushoto ni) Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Dkt, Zabron Masatu pamoja na Meneja Mradi wa Mama na mtoto, Tanya Salewski (kulia)
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.