Miradi ya Boost inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kuidhihirisha dhamira yake ya dhati katika kuboresha sekta ya elimu nchini kwa kutoa fedha za BOOST kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Dkt. Chrispine Shami,
Hatua hii inalenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na kuongeza fursa za elimu bora kwa watoto wa wilaya hiyo, kupitia mpango huo, jumla ya shilingi bilioni 1,282,079,136/= mwaka 2024/2025 zimetolewa kwa ajili ya kugharamia ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za awali na msingi, fedha hizo ni mchango mkubwa katika kuimarisha huduma za elimu na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wa Misungwi kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa tarehe 9 Januari 2026 wakati wa ufuatiliaji na ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayoendelea kutekelezwa wilayani humo kwa lengo la kujiridhisha na hatua za utekelezaji wa miradi, ubora wa kazi pamoja na matumizi sahihi ya fedha za umma kwa maslahi ya wananchi.
Akizungumza katika ukaguzi wa miradi hiyo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Dkt. Chrispine Shami, alisema kuwa hakuna sababu ya kukwamisha utekelezaji wa miradi kwa visingizio visivyo na msingi, amesisitiza kuwa miradi hiyo ni ya wananchi, hivyo lazima ikamilike kwa wakati ili iweze kuleta tija iliyokusudiwa mapema.
Dkt. Shami aliwataka watendaji wa Halmashauri, wakandarasi pamoja na vibarua kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba waliyoingia na alieleza kuwa uwajibikaji na uadilifu katika utekelezaji wa miradi ni muhimu ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora baada ya miradi hiyo kukamilika.
Naye Kaimu Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Bi. Mwanajumbe Zuberi, alieleza kuwa miradi iliyokaguliwa inatekelezwa kwa fedha za BOOST katika kata mbalimbali ikiwemo Kata ya Koromije, ambapo kuna ujenzi wa shule mpya ya awali na msingi Kigara pamoja na ukarabati wa Shule ya Msingi Ibongoya ‘A’ kwa gharama ya shilingi 462,179,136.00.
Ameongeza kwamba katika Shule ya Sekondari Gambajiga, kuna ujenzi wa shule mpya ya awali na msingi utakaogharimu shilingi 330,700,000.00, aliitaja Miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa na vyoo vyenye matundu sita katika Shule ya Msingi Busagara, Kata ya Usagara, kwa gharama ya shilingi 138,600,000.00.
Katika Kata ya Idetemya, Serikali imefanya ukarabati wa miundombinu ya Shule ya Msingi Bukumbi kwa shilingi 121,000,000.00 na Shule ya Msingi Kigongo kwa shilingi 141,000,000.00 Vilevile, ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na choo chenye matundu sita katika Shule ya Msingi Seth-Benjamin umetengewa shilingi 88,600,000.00, fedha zote zikitokana na mpango wa BOOST.

Kwa upande wao, timu ya Menejimenti ya Halmashauri wamewataka Wataalam na wasimamizi wa miradi kusimamia utekelezaji kwa weledi na uwajibikaji mkubwa, huku wakiwahimiza wananchi kushiriki katika ulinzi na utunzaji wa miradi hiyo, ushirikiano kati ya Serikali na wananchi umeelezwa kuwa ni nguzo muhimu ya kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora unaotakiwa na kuleta maendeleo endelevu katika sekta ya elimu wilayani Misungwi.
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Misungwi akiwemo Bw. John Nyanda Mkazi wa Kijiji cha Gambajiga ameeleza kuridhishwa kwao na utekelezaji wa miradi ya elimu inayofadhiliwa kupitia fedha za BOOST, amesema kuwa miradi hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa watoto wao na jamii kwa ujumla. Baadhi ya wananchi wamesema ujenzi wa shule mpya na ukarabati wa miundombinu ya shule za awali na msingi utapunguza umbali wanaotembea watoto kwenda shule, kuongeza usalama wao na kuboresha mazingira ya kujifunzia, jambo litakalosaidia kuinua kiwango cha elimu katika wilaya hiyo.
Wakati huo huo Wananchi wameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuwekeza kwenye sekta ya elimu na kusikiliza mahitaji ya wananchi wa maeneo ya vijijini, hata hivyo, wametoa maoni yao wakitaka miradi hiyo isimamiwe kwa karibu ili ikamilike kwa ubora na kwa wakati uliopangwa, huku wakiahidi kushiriki kikamilifu katika ulinzi na utunzaji wa miundombinu hiyo ili idumu na kuendelea kuwanufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.