Serikali ya awamu ya tano imepanga kutoa shilingi Billioni 1.5 katika mpango wa awamu ya pili za Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza ili kuboresha utoaji wa huduma za Afya kwa Wananchi na kupunguza msongamano wa wagonjwa wengi kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-toure.
Mhe,Waziri Mkuu ,Kassim Majaliwa alitoa ahadi hiyo ya Serikali wakati akizungumza na Wananchi wa Koromije Wilayani Misungwi katika ziara yake kwa lengo la kufuatilia utekelezaji na ufunguzi rasmi wa mradi wa ujenzi na ukarabati mkubwa wa Kituo cha Afya Koromije uliogharimu fedha zaidi ya shilingi Milioni 500 zilizotolewa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI ambapo Majengo matano yamekamilika ikwemo jengo la Maabara, Upasuaji, Wodi ya Wazazi,Nyumba ya Mganga na jengo la kuhifadhia maiti,sambamba na kujenga majengo hayo matano Halmashauri imefanikiwa kujenga na kukamilisha jengo la ziada la X-ray kutokana na fedha zilizotolewa.
Mhe,Waziri Mkuu wa Tanzania alifurahishwa sana na kuwapongeza Kamati ya ujenzi ,Viongozi wa Wilaya, Kata na Kijiji na wananchi wote kwa kushiriki na kusimamia kikamilifu ujenzi na ukarabati huo uliofanywa kwa kiwango na ubora, na kuwaomba wananchi kuiamini Serikali ya awamu ya tano ambayo imeweka mkakati madhubuti wa kuboresha na kuimarisha utoaji wa huduma bora za Afya nchini kote, “tayari Vituo vya Afya 340 vimejengwa na kukarabatiwa nchi nzima na Serikali inaendelea kutoa fedha zingine kwa awamu ya pili za ujenzi wa Zahanati na Vituo vya Afya na fedha za ununuzi wa madawa na vifaa tiba kwa malengo mapana ya kuboresha huduma za upasuaji mdogo na mkubwa na . Alisema Waziri Mkuu Majaliwa”.
Baadhi ya wananchi wa Koromije wakimsikiliza Waziri Mkuu wakati wa ufunguzi wa kituo cha afya Koromije
Amewaagiza Viongozi wa Halmashauri ya Misungwi kwa kushirikiana na Vijiji kuhamasisha na kuanzisha pamoja na kusimamia ujenzi wa Zahanati katika kila Kijiji ambao ni ujenzi wa angalau vyumba vitano tu muhimu kwa ajili ya utoaji wa huduma za Afya za awali kwa Magonjwa ya kawaida , pamoja na kuongeza majengo mengine ya Wodi ya Wanaume na Wodi ya watu wenye magonjwa mchanganyiko katika Kituo cha Afya cha Koromije ili kuwezesha wananchi wengi kupata huduma bora za Afya kwa ukaribu na haraka zaidi, na alitoa onyo kwa Madaktari na Watumishi wa Afya wenye tabia ya kuwaelekeza Wagojwa kununua madawa katika maduka binafsi na kuwataka waache mara moja vitendo hivyo ambavyo ni kinyume na maadili ya taaluma yao na kanuni za utumishi wa umma.
Mwonekano wa nyuma wa jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya Koromije
Mhe,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akitoa maelezo kuhusu hoja na kero ya uhaba wa maji maeneo ya Koromije iliyotolewa na Diwani wa Kata ya Koromije Mhe.Bilarmin Hilary, alisema Serikali imepanga kutoa fedha za kutekeleza mradi wa maji katika mpango wa Vijiji 17 na kuagiza Mhandisi wa Mkoa kuviunganisha Vijiji vya Kata ya Koromije ili kuondoa adha na kero ya kukosa maji wanayoipata.
Mhe,Waziri Mkuu alionyeshwa kukerwa na suala la Wananchi kukata miti na misitu ovyo sambamba na kuharibu vyanzo vya maji na kwamba ni vitendo ambavyo vinasababisha kukosekana kwa maji ardhini, “ Wananchi acheni tabia ya kukata miti ovyo na Viongozi wa Kata na Vijiji simamieni suala la utunzaji wa mazingira pamoja na vyanzo vya maji”.Alikemea Waziri Mkuu.
Aliwataka Wazazi kuwaandikisha na kuwapeleka Shule watoto katika darasa la awali na darasa la kwanza pamoja na kuwahudumia kwa kuwapa mahitaji muhimu ya vifaa vya shule, madaftari, sare na viatu ili kuwawezesha kusoma kwa bidii na Serikali itaendelea kutoa fedha za elimu bila malipo kwa shule zote za Serikali nchini, na amewatka Viongozi wa ngazi ya Wilaya kuhakikisha wanajiridhisha na kupata takwimu halisi ya kila shule ya msingi kuwa na darasa la awali lililo na wanafunzi, hata hivyo aliwatoa wasiwasi Wananchi kuhusu kuchangishwa michango isiyokuwa muhimu kwa ajili ya maendeleo ya shule na kwamba suala la michango ni maamuzi ya Wazazi kwa kushirikiana na Halmashauri pamoja na Wakuu wa Wilaya.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi katika Mradi wa Maji Safi wa Nyahiti Misungwi(kushoto) Mhe,John Mongella Mkuu wa Mkoa wa Mwanza akishuhudia tukio hilo
Awali, Mhe, Waziri Mkuu aliweka Jiwe la Msingi katika ujenzi wa mradi mkubwa wa Maji safi wa Nyahiti –Misugwi unaotekelezwa na Kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction Cooperation CCECC) chini ya Mhandisi Mshauri Kampuni ya Egis ya Ufaransa na mradi huo unasimamiwa na Mamlaka ya Maji safi na usafi wa Mazingira MWAUWASA) ambao utagharimu shilingi Bilioni 12.85 na mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Mei mwaka huu.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.