Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani aagiza Tannesco kuhakikisha wanaweka Transforma kubwa katika Mgodi wa Busolwa Mining Group pamoja na maeneo ya Kata ya Usagara kabla ya tarehe 15 Januari mwakani.
Akizungumza katika ziara yake ya kutembelea na kukagua maeneo ya Mgodi wa Busolwa Mining Group Wilayani Misungwi ambayo yanahitaji huduma ya umeme, Waziri Kalemani amesema kwamba ni muhimu sana kwa Wawekezaji kufanya kazi na kuendesha shughuli zao katika miundombinu bora na salama na kuagiza Shrika la Tannesco kuhakikisha wanapeleka Transforma yenye uwezo unaotakiwa katika Mgodi huo kabla ya tarehe 15 Janauri mwaka 2021 ili kuwezesha wawekezaji hao kuzalisha vizuri na kwa gharama nafuu.
Dkt, Kalemani amesema kuwa ni wakati sasa umefika ambapo maeneo ya Migodi yote nchi nzima yapitiwe na kuhakikisha wanapata miundombinu ya umeme kwa wakati ili kuwapunguzia gharama za uendeshaji kwa kutumia mafuta ya Generator na hivyo kuongeza na kuleta maendeleo.
Waziri Kalemani amesema kwamba Serikali imefanya kazi kubwa katika kusambaza umeme na kueleza kwamba kuna maeneo ambayo bado hayajapata umeme katika vijiji vya Kata ya Usagara Wilayani Misungwi kutokana na ukosefu wa Transforma na kuiagiza Tannesco Kanda ya Mwanza kuhakikisha wanaweka Transforma katika maeneo hayo mapema na kusambaza umeme kwa wakati.
Wakati huo huo Serikali itaanzisha mradi wa Vitongoji mwezi Februari mwakani ambao utatekelezwa kwa kuweka umeme katika Vitongoji vyote nchini kwa muda wa miezi 15, ambapo ameitaka Tannesco kukamilisha uwekaji wa umeme katika vijiji 36 vilivyobaki vya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi katika mradi huo na kuwahakikishia Wananchi kwamba hakuna mtu atakayerukwa katika mradi huo.
Awali akiwasilisha taarifa ya Wilaya ya Misungwi, Katibu Tawala Wilaya, Petro Sabatto kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda ambaye alieleleza kwa kuishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa kufanikisha kusambaza umeme katika maeneo mengi kwa Wilaya ambayo ina Kata 27 na Vijiji 114 ambapo hadi sasa ni Kata tatu tu ambazo havijaunganishwa na umeme ambazo ni Kata ya Isenengeja, Lubili na Shilalo.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (wa pili kulia) akikagua na kuona maeneo ya uwekezaji wa Madini katika Mgodi wa Madini wa Busolwa Mining group Wilayani Misungwi katika ziara hiyo aliambatana na Naibu Waziri wa Nishati Steven Byabato wa kwanza kulia wakiwa pamoja na Mkurugenzi wa Kampuni ya Busolwa Mining Group Baraka na Viongozi wengine wa Tannesco Kanda ya Mwanza.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.