Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jaffo aridhishwa na hatua ya ujenzi uliokamilika wa Majengo mawili ya Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.
Akizungumza katika ziara yake ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi inayojengwa katika Kijiji cha Iteja na Mwamanga Waziri Jaffo amepongeza na kuwasifia Viongozi na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa juhudi walizofanya katika kusimamia hatua zote za ujenzi wa majengo mawili ya maabara na jengo la Wagonjwa wa nje ambayo yamejengwa kwa gharama ya shilingi Milioni 488.6 hadi kukamilika kati ya fedha zilizotolewa na Serikali shilingi milioni 500.
“Kwa hiyo Mkuu wa Mkoa katika Jengo lililosimamiwa vizuri ni hili hapa , na hapa nimeridhika sana manake maeneo mengine watu wanaweka bati reject lakini hapa kila eneo ni safi na Wasukuma wenzangu hapa watafurahi sana watatamani kuumwa tu hata kama wamegombana na waume au wake zao ”. Alisisitiza Waziri Jafo
Waziri Jafo amesema kwamba jengo la Misungwi limesimamiwa vizuri sana Jengo la Misungwi katika kila eneo ukiangalia milango, vyoo hadi paa vyote ni vizuri tu, jingo ni zuri sana, nimeona hadi chooni ukimwaga maji yanatiririka na kueleza kwamba atapeleka salam kwa Mhe, Rais ili aweze kuongeza fedha za kuendelea na ujenzi na kukamilika kwa Hospitali.
Waziri Jafo ameongeza na kupongeza ushirikiano uliopo baina ya Viongozi wa Wilaya na Watendaji wa Halmashauri ambao ndio umefanikisha kazi kubwa ya ujenzi kufanyika na kuomba maeneo mengine kuiga mfano huo na kutekeleza miradi kwa kiwango na ubora mzuri unaokubalika na kuonekana.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela alishukuru sana kwa Serikali ya awamu ya tano kwa kutoa fedha za miradi mbalimbali ikwemo na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya na kuahidi kuendelea kusimamia kikamilifu miradi mingine inayoendelea.
Awali akiwasilisha taarifa ya ujenzi Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya Dkt, Raymond Nyasebwa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri alieleza kwamba utekelezaji wa ujenzi huu ulianza tarehe 11/06/2020 kwa majengo mawili yaani ujenzi wa Maabara na Jengo la wagonjwa wa nje (OPD).
Dkt. Nyasebwa amesema kuwa Halmashauri imetekeleza ujenzi huu kwa kutumia njia ya “Force account” kwa kusimamia ujenzi chini ya Wahandisi wa Halmashauri kwa kutumia watalaamu na vifaa vyake, kuajiri mafundi/vibarua wa muda na kushirikisha Jamii, mradi huu umenufaisha wananchi 156 kwa kupata ajira ya muda mfupi na kuongeza kipato chao.
Alisema jumla ya shilingi milioni 488,671,134. zimetumika kununua vifaa vya ujenzi na kulipa mafundi kwa ajili ya majengo yote mawili na kubakiwa na kiasi cha shilingi milioni 11,328,866 hadi sasa utekelezaji wa mradi kwa majengo yote mawili yaani Maabara na jengo la wagonjwa wa nje - OPD umekamilika kwa asilimia 98, aidha Halmashauri inategemea kuanza kutoa huduma mapema mwezi Februari 2021.
Mwonekano wa Jengo la Wagonjwa wa nje OPD ambalo limejengwa katika Hospitali mpya ya Wilaya ya Misungwi.
Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa,(TAMISEMI) Selemani Jafo (katikati) akikagua na kuona maeneo ya ndani ya ujenzi wa Jengo la Wagonjwa wa nje lililojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi mapema jana (Kulia ni) Mkuu wa Mkoa wa Mwanza John Mongela akifuatiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Kisena Mabuba (Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda wakiwa katika ziara hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.