Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2022 Sahili Geraruma awashauri Watanzania Wazawa kutumia fursa za maeneo na rasilimali zilizopo nchini kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Wito huo umetolewa mapema jana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru wakati akikagua na kuweka Jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha Afya cha MacWish kilichopo katika Kijiji cha Nyang’homango Kata ya Usagara katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ambacho hadi kukamilika kitagharimu fedha shilingi Bilioni 1.5.
Bw. Geraruma aliwataka Watanzania kutumia fursa zilizopo katika uwekezaji na kuendeleza sera ya Serikali ya awamu ya sita ya kutumia Wazawa kuwekeza katika maeneo ya sekta mbalimbali kwa lengo la kutatua na kupunguza changamoto ya ajira kwa Vijana kwa kuzalisha ajira za kutosha hapa nchini.
Naye Mkurugenzi wa Chuo hicho Bw,Patrice Makasi ametoa rai na kuwaomba Wananchi kutoa ushirikiano katika kuwekeza, kuleta maendeleo na kukuza uchumi katika sekta ya uwekazaji na kuwahakikisha kwamba watazalisha Wataalamu wenye viwango bora ndani ya nchi na nje ya nchi katika kada ya Afya ili kuleta ushindani katika soko la ajira.
Aliongeza kwamba katika mikakati ya Chuo hicho katika mipango ya utoaji wa elimu bora kina uwezo wa kudahili Wanafunzi 1,500 kwa mwaka huu wa masomo 2022/2023 wanatarajia kudahili Wanafunzi 250 katika kozi ya Ufamasia na Utabibu na kusisitiza Watanzania kutumia fursa za masomo katika Chuo hicho.
Kwa upande wake Afisa wa Masoko wa Chuo hicho Bw,Boniphace Mwaliki amesema kuwa lengo kubwa ni kuandaa Wataalamu wa Afya wenye ubora wa kimataifa wenye kuleta tija katika soko la ajira na kusisitiza kuwa ulipaji wa ada ni nafuu unaweza kulipa kwa awamu nne ,na wamezingatia ubora katika utoaji wa Elimu hapa nchini.
Wakati huo huo, Mbunge wa Jimbo la Misungwi Mhe, Alexander Mnyeti amebainisha kwamba Serikali ya awamu ya sita katika mwaka wa fedha 2021/2022 imetoa takribani shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya sekta ya Afya fedha ambazo zimetumika kujenga miundombinu ya majengo ya Hospitali,ya Wilaya, Kituo cha Afya cha Usagara na baadhi ya Zahanati.
Ametoa shukrani za dhati kwa Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha ambazo zimeweza kutekeleza mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Usagara ambacho kimewekewa jiwe la msingi kilichogharimu shilingi 257,950,000/= ambapo majengo yaliyojengwa ni pamoja na jengo la Wagonjwa wa nje (OPD) , jengo la Maabara, na Kichomea taka.
Naye mkazi wa Usagara Bw,Faustine Joseph ameishukuru Serikali kwa kujenga Kituo cha Afya Usagara na kwamba kitarahisisha kupatikana kwa huduma ya Afya kuwa karibu na wananchi na kuondoa adha ya umbali kwenda kutafuta huduma maeneo ya mbali na kusafiri kwa umbali mrefu kwenda Misungwi , Bukumbi hospitali na Butimba Mwanza mjini kutafuta huduma ya matibabu hivyo kwa kupata Kituo hiki cha Afya kitasaidia kuondoa adha hiyo kwa wakazi wa Usagara.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2022 katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi zimeweza kupitia Miradi saba yenye thamani ya Bilioni 3.2 yote ikiwa katika hali nzuri ya utekelezaji na imejengwa kwa kiwango na ubora.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Bw,Sahili Geraruma (kushoto) akikagua Mradi wa Ujenzi wa Chuo Cha Afya MacWish kilichopo kijiji cha Nyanghomango Kata ya Usagara wakati wa uwekaji wa jiwe la Msingi,kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe,Veronika Kessy.
Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Bw,Sahili Geraruma(wa pili kutoka kulia) akiwa na Wakurugenzi wa Chuo cha MacWish Bw. Ernest Wish( wa kwanza kulia) na Patrice Makasi( wa tatu kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa Uwekaji wa Jiwe la Msingi.an Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe, Veronika Kessy.
Bw. Edward Wish ((kushoto) ambaye ni Baba mzazi wa Wakurugenzi wa Chuo cha Afya cha MacWish akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru 2022 akiwa katika picha ya pamoja wakati wa uwekaji wa jiwe la Msingi Chuo cha MacWish pamoja na Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2022 Bw,Sahili Geraruma wa pili kulia, na katikati ni Mkuu wa Wilaya Mhe, Veronica Kessy,wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misungwi Mhe, Kashinje Machibya.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.