Wazazi na Wananchi wahamasishwa na kushauriwa kuwaandaa na kuwaruhusu Watoto wa umri wa miaka 5 hadi 14 kupata Dawa ya matibabu ya Ugonjwa wa Minyoo na Kichocho Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe, Paulo Chacha kupitia kwa Mwakilishi wake Afisa Tawala Wilaya ya Misungwi Bw. Jonas Kamugisha ambaye amewataka Viongozi na Watendaji kutoa elimu na kuhamasisha jamii na Wazazi kuwaruhusu Watoto kujitokeza kupata Dawa ya kuua wadudu wa Kichoo na Minyoo
Mhe, Kamugisha ambaye ni Afisa Tawala Wilaya ameyasema hayo katika kikao cha Kamati ya Afya ya msingi ya Wilaya kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa ajili ya kuweka mikakati na maandalizi ya utoaji wa Dawa ya matibabu ya Ugonjwa wa Kichocho na Minyoo amabyo hutolewa kwa watoto wote wa umri kuanzia miaka 5 hadi 14.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bw. Christopher Legonda amesema na kuwataka Viongozi na Watendaji kuendelea kuhamasisha na kutoa elimu kwa Wananchi ili kuongeza ulewa wa namna ya kuchukua tahadhari na kujikinga na maambukizi ya magonjwa ya kuambukiza na magonjwa ya mlipuko ikiwemo ugonjwa wa Kipindupindu ambao umeshaanza kutokea katika maeneo mengine ya Mikoa jirani ya Mara na Simiyu sambamba na kuwashauri Wazazi wote kutoa hamasa kwa watoto kujitokeza kupata dawa ya Minyoo na Kichocho katika vituo vilivopangwa kwenye shule za msingi na Sekondari siku ya Ijumaa na Jumamosi wiki hii..
Naye, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Dkt. Clement Morabu ametoa rai kwa Viongozi na Watendaji kuendelea kutoa elimu na hamasa kwa Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga na maambukizi ya magonjwa mbalimbali yakiwemo ya kuambukiza na magojwa ya mlipuko na kushauri Wananchi kutunza mazingira,kufuata na kuzingatia kanuni bora za Afya na kuzingatia maelekezo na ushauri unaotolewa na Wataalam wa Afya.
Dkt. Morabu amesema kwamba kuna umuhimu mkubwa jamii ikafahamu kuhusu namna magonjwa haya ya Kichocho na Minyoo yanavyoambukizwa na kusababisha athari katika mwili wa binadamu ikiwemo kuharibu ini, na kusababisha Kansa ya utumbo, alieleza baadhi ya aina ya Kichocho na athari zake na kwamba Serikali imeweka mpango na Kampeni yaa kutoa dawa ya matibabu ya Ugonjwa Kichocho na Minyoo kwa watoto wote kuanzia umri wa miaka 5 hadi 14 na zoezi hili linafanyika mwezi Novemba kwa kila mwaka kabala ya Wanafunzi hawajafunga shule.
Dkt. Morabu amewasihi Viongozi na Watendaji hao kuendelea kutoa elimu kwa Wazazi na Wananchi kuwaruhusu watoto kujitokeza kupata dawa hizo na kuwaomba Wazazi na Walimu wa Shule za msingi na Sekondari kuwandaa watoto kikamilifu kwa kuwapatia chakula cha kutosha kuweza kuhimili uwezo wa dawa mwilini ambapo utaratibu wa utoaji wa Dawa hizo hutolewa kwa kuzingatia uzito wa mtoto mwenyewe.
Wakati huo huo, Afisa Afya wa Wilaya ya Misungwi Bw. Dismas Dotto ametoa elimu katika mada ya Mlipuko wa Ugonjwa wa Kipundupindu na kuwakumbusha Wajumbe kuhusu majukumu yao ikiwemo kuhamasisha na kutoa elimu kwa Wananchi kuhusu kujikinga na maambukizi pamoja na kuwa tayari na kukabiliana na mlipuko wa magonjwa mbalimbali ikiwemo Ugonjwa wa Kipindupindu uliojitokeza hivi karibuni mwaka huu katika Mikoa 6 na baadhi ya Wananchi waliambukizwa ambapo kwa sasa hakuna Mgonjwa mpya ambaye ametolewa taarifa.
Bw. Dotto amebainisha baadhi ya mikakati ambayo Wilaya imeendelea kuchukua ni pamoja na kuhamasisha Wananchi kujenga vyoo,Wananchi kuendelea kunawa mikono mara kwa mara, kuendelea kuchemsha maji na kuweka mazingira ya majumbani katika usafi, ili kuweza kuepuka na kukabiliana na Magonjwa ya mlipuko ikiwemo Ugonjwa huu wa Kipindupindu.
Badhii ya Wajumbe walioshiriki katika kikao hicho ni pamoja na Viongozi wa Madhehebu ya Dini, Wataalam na Watendaji wa Idara ya Afya, Elimu, Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa jamii , Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Maafisa Afya na Maafisa Tarafa wote wa Wilaya ya Misungwi kwa lengo la kuwapa uelewa na kuweza kupeleka elimu katika jamii na kuongeza hamasa kwa Wananchi juu ya masula ya kujikinga na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza na magonjwa ya mlipuko.
Baadhi ya Wajumbe walioshiriki katika kikao hicho na Viongozi wa madhehebu ya Dini katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Novemba,22,2023
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Dr.Clement Morabu akitoa maelezo juu ya zoezi la kupatiwa dawa za Minyoo na Kichocho kwa Watoto wenye umri wa miaka 5 hadi 14 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Novemba,22,2023.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.