Watendaji wa Kata na Vijiji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi watakiwa kusoma taarifa za Mapato na Matumizi katika Mikutano ya kisheria ya kila robo mwaka ili kuleta ufahamu na uelewa kwa Wananchi kuhusu fedha zinazotolewa na zinavyotumika katika utekelezaji wa miradi katika maeneo yao.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe, Juma Sweda ametoa agizo hilo wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Ngudama katika Kata ya Bulemeji baada ya kukamilisha Ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya sekta mbalimbali inayotekelezwa katika vijiji vya Kata hiyo kwa ufadhili wa fedha za Serikali,Wahisani pamoja na michango na nguvu za Wananchi.
Mhe,Juma Sweda amewataka Watendaji wa Kata na Vijiji wote kufanya kazi na kuwajibika kikamilifu hususani kusoma taarifa za Mapato na Matumizi ya fedha zote zinazotolewa na Serikali,Wafadhili na Wahisani mbalimbali pamoja na michango na nguvu za Wananchi kwa lengo la kuongeza uwajibikaji, uwazi na kuleta imani kwa Wananchi kushiriki katika kuchangia na kutekeleza miradi mbalimbali na kuona na kuhakikisha namna fedha hizo zinavvotumika kutekeleza vizuri miradi husika na hatimaye kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Wananchi.
Amewataka pia Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Vikao na Mikutano hiyo ya vijiji kwa ajili ya kujadili ajenda ya taarifa ya mapato na matumizi na kuwaomba washirikiane na Kamati za Siasa za Kata na Vijiji ili kutekeleza ipasavyo Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 na Viongozi hao wa Chama wahakikishe Ilani inatekelezwa vizuri katika sekta zote, “ na huo ndio utaratibu na kanuni za Chama cha Mapinduzi katika kuwaletea maendeleo Wananchi wake” Alisisitiza Mkuu wa Wilaya, Juma Sweda.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,Mhe, juma Sweda akihutubia Wananchi wa Kijiji cha Ngudama Kata ya Bulemeji wakati wa Mkutano wa hadhara uliofanyika katika maeneo ya Viwanja vya Ngudama.
Mhe,Sweda amewataka Wananchi kutumia fursa ya Kilimo na kuandaa mashamba kikamilifu kwa kuweka mbolea aina ya Samadi na kulima kwa wakati mara msimu wa mvua utakapoanza kwa kuzingatia kanuni bora za Kilimo na ushauri wa Wataalam wa Ugani /Kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao ya Chakula na Biashara na hatimaye kuongeza kipato na uchumi wa Kaya na jamii kwa ujumla.
Baadhi ya Wananchi na wakazi wa Kijiji cha Ngudama,Kata ya Bulemeji wakisikiliza kwa makini maelekezo na maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kwenye Mkutano wa hadhara
Amewaasa Wananchi hao kutouza ardhi na mashamba yao kiholela na badala yake wavute subira na kuyatunza kwa manufaa na faida kubwa ya baadae kutokana na kupanda kwa thamani ya ardhi na kuwaomba wapime maeneo hayo kupitia sera ya upimaji shirikishi inayoendelea kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Makampuni binafsi ya upimaji wa Ardhi kwa lengo la kutekeleza na kufikia adhima ya jenzi wa uchumi wa Viwanda.
Mhe,Juma Sweda amewahamasisha na kuwataka Wananchi wa rika mbalimbali kuanzisha na kujiunga katika vikundi mbalimbali vya uzalishaji mali na kutumia fursa ya Mikopo inayotolewa na Serikali kupitia makundi ya akinamama, Vijana na watu wenye ulemavu na kuweza kunufaika na kufaidika na mikopo ya fedha hizo kuanzisha miradi mbalimbali ya kuinua kipato na kukuza uchumi katika jamii.
Awali katika ziara yake Mkuu wa Wilaya huyo na Kamati ya Ulinzi na Usalama pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo walitembelea na kukagua shughuli na kuona utekelezaji wa miradi ya sekta mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Kisima cha Maji katika Kijiji cha Mwalwigi, Ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Sekondari ya Kata ya Mamaye na kuona Vikundi vya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Kata ya Ukiriguru, ujenzi wa mabweni na Ukamilishaji wa miundombinu ya Maabara katika Shule ya Sekondari ya Paulo Bomani, Ujenzi wa Jengo la Zahanati ya Kijiji cha Nyamatala, Kata ya Ukiriguru.
Jengo la Maabara tatu za Sayansi lililojengwa katika Shule ya Sekondari Paulo Bomani Kata ya Ukiriguru na sasa linaendelea kukamilishwa..
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe, Juma Sweda akishiriki kupaka rangi kwenye ukuta wa ndani ya Jengo la Maabara yanayoendelea kukamilishwa kwa gharama ya shillingi Millioni 50 zilizotolewa na Serikali hivi karibuni katika Shule ya Sekondari Paulo Bomani Kata ya Ukiriguru.
Vile vile, wameweza kukagua na kuona ujenzi wa Choo katika Shule ya Msingi Mwalogwabagole na ujenzi wa Nyumba ya Mtumishi katika Zahanati ya Buhunda pamoja na kukagua shughuli za mradi wa Uzalishaji mali wa Kikundi cha akinamama cha Ngudama ambapo Mkuu wa Wilaya alipongeza juhudi za Kikundi hicho cha akinamama ambao wanatengeneza bidhaa za asili vya matumizi ya Nyumbani na kuwasihi waendelee na kazi hiyo na wengine waige na kujiunga kwenye vikundi vya ujasiliamali.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.