Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi amewataka Wananchi kuhakikisha wanazingatia sheria, taratibu na kuepuka kujichukulia sheria mkononi na kupaswa kuendelea kutoa ushirikiano kwa Kamati ya Usalama Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Mhe. Samizi ametoa rai hiyo Leo Tarehe 20 Septemba 2025 katika Mkutano na Wananchi wote wa kijiji cha Manawa na kijiji cha Ndua kwa nyakati tofauti ambapo ametoa maelekezo maalumu juu ya mgogoro uliokuepo kati ya wakulima na wafugaji katika vijiji hivyo vilivyopo Tarafa ya Innonerwa, Mgogoro huo umekuwa ukijitokeza mara kwa mara kutokana na malalamiko ya uharibifu wa mazao unaosababishwa na mifugo pamoja na madai ya wakulima kuhusu uvamizi wa maeneo yao kwa kisingizio cha kukosa malisho na maji kwa mifugo yao.
Akizungumza na Wananchi wa Tarafa hiyo katika mkutano wa hadhara, Mhe Samizi amewataka wakulima na wafugaji kuishi kwa amani na kuheshimiana, huku akisisitiza umuhimu wa kila Mwananchi analisha mifugo katika eneo lake pasipo kuingia katika eneo la mwingine au kijiji kingine pia ameagiza viongozi wa vijiji na vitongoji kuhakikisha wanashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudhibiti mifugo isiingie kwenye mashamba.
Aidha, amewataka maafisa mifugo na kilimo katika wilaya hiyo kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi juu ya matumizi bora ya ardhi na kuhamasisha ufugaji wa kisasa utakaopunguza migongano. "Ni wajibu wetu kulinda amani na mshikamano, hatutakubali mtu yeyote kuendeleza uhasama unaoweza kusababisha madhara makubwa katika jamii," alisema Mkuu wa Wilaya.
Katika hatua nyingine Mhe. Samizi amewahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani ifikapo tarehe 29 Octoba 2025 kwani ni haki ya kila mwananchi kupiga kura.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Misungwi OCD Gasper Silayo amewasisitiza wananchi hao kuhakikisha wanaepuka viyendo vya uhalifu wa aina yoyote vinavyoweza kuvunja amani na kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuwabaini wahalifu hao.
Wananchi waliohudhuria mkutano huo wamepongeza hatua ya Serikali kushughulikia suala hilo, wakieleza kuwa maelekezo yaliyotolewa yatawezesha kuimarisha mshikamano na kupunguza migongano ya mara kwa mara.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.