Jumla ya Watahiniwa 7,776 wanatarajiwa kufanya Mitihani ya kumaliza Elimu ya Msingi kuanzia tarehe 11 hadi 12 mwezi Septemba mwaka 2019 katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Bw, Frank Magabiro ameeleza haya kwa Waandishi wa Habari ofisini kwake mapema leo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Bw, Kisena Mabuba, alisema kwamba Halmashauri hiyo imeshafanya na kukamilisha maandalizi yote ya zoezi la kitaifa la uendeshaji wa Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi kwa Wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2019.
Bw, Magabiro amesema kwamba kuna jumla ya Watahiniwa 7,776 waliosajiliwa kwa ajili ya kufanya Mtihani huo wa kumaliza Elimu ya msingi kwa mwaka 2019, ambapo Wavulani ni 3,596 na Wasichana ni 4,180 na tayari maandalizi ya msingi na mambo mengine yapo vizuri hususani suala la usafiri na usambazaji wa Mitihani kuelekea katika Vituo 146.
Bw, Frank Magabiro Afisa Elimu Msingi, wa Halmashauri ya wilaya ya Misungwi, akizungumza na Wanahabari ofisini kwake mapema jana,
Mwl, Twaha Hussein Said ambaye ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mbela, akizungumza ofisini kwake na Bw, Frank Magabiro Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Misungwi, wakati alipotembelea Shuleni hapo kuona maandalizi ya msingi ya zoezi la Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi inayotarajiwa kufanyika tarehe 11 na 12 mwezi Septemba 2019.
Bw, Magabiro alifafanua kuwa kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania inaeleza kwamba Mitihani hiyo ya kumaliza Elimu ya Msingi itaanza siku ya Jumatano kuanzia saa 2.00 asubuhi kwa watahiniwa kufanya masomo ya English Language , Hisabati na Maarifa ya jamii na kukamilika siku ya Alhamisi kwa Watahiniwa kufanya masomo ya Kiswahili na Sayansi.
Afisa Elimu huyo ameongeza kuwa kwa upande wa Watahiniwa wa Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka huu 2019 kumekuwepo na ongezeko la Watahiniwa 188 ambayo ni sawa na asilimia 2.4 ya Watahiniwa 7,588 waliohitimu Elimu ya Msingi mwaka jana 2018 katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Bw, Frank Magabiro amebainisha sababu iliyowezesha kuongezeka kwa Watahiniwa hao ni pamoja na udhibiti wa utoro kwa Wanafunzi, mwitikio wa Wazazi na jamii katika suala la Elimu sambamba na utekelezaji wa Sera ya Serikali ya utoaji wa Elimu bila malipo ambayo inatekelezwa katika Shule zote za msingi 147, zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi zikwemo Shule za Serikali 139 na shule binafsi 8.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya Wanafunzi katika masomo, Bw, Magabiro alisema kwamba Wanafunzi wote wameendaliwa vizuri kimasomo ambapo mada zote zilizopaswa kufundishwa zote zilikamilishwa, na wamefanya majaribio ya kutosha pamoja na Mitihani mbalimbali ya ngazi ya Kata, Wilaya sambamba na Mtihani wa MOCK Mkoa, pia wamejengwa vizuri kisaikolojia na Walimu pamoja na Wazazi ‘’ameongeza kuwa kimsingi Watahiniwa wote wapo tayari kufanya Mitihani hiyo’’. Alisisitiza Bw, Magabiro.
Bw, Magabiro amewataka Watahiniwa hao kuwa watulivu na kutambua kwamba Mtihani huo wa Taifa ni sawa na Mitihani mingine na kuwatakia kheri na Afya njema wakati wote na kuwaomba wamtangulize Mungu awasaidie katika Mitihani hiyo muhimu.
Bw, Frank Magabiro Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Misungwi, akizungumza na baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mbela katika Kata ya Misungwi, ambayo ina Watahiniwa 167 watakaofanya Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka huu 2019, amewaasa na kuwatia moyo na kuwatakia kheri katika Mitihani yao na kuwaomba kuwa waaminifu.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.