Viongozi,Wananchi watakiwa kuitunza vizuri Miundombinu ya Miradi ya Elimu Jumuishi kwa manufaa ya wanafunzi Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Wito huo umetolewa jana 7, Desemba, 2023 na Afisa Msimamizi wa Elimu maalumu OR-TAMISEMI Bi.Anna Mark katika hafla fupi ya kukabidhi ukarabati wa vyumba 7 vya madarasa na Ujenzi wa matundu ya vyoo mara baada ya kukamilika iliyofanyika katika Shule ya Msingi Mabuki chini ya Mradi wa Elimu Jumuishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ambapo amewataka Wananchi na wadau mbalimbali kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Aidha Bi.Mark amesema kuwa vifaa vinatolewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu ni kwa ajili ya watoto wote wenye mahitaji maalumu waliobainishwa na wataalamu kutoka ngazi ya Halmashauri vifaa hivyo ni vya kujifunzia na vifaa saidizi kama viti vya magurudumu pamoja na vifaa vya kukuza maandishi kwa wale wenye uoni hafifu.
Mkurugenzi wa Sense International Tanzania Bi.Naomi B Lugoe amesema kuwa baadhi ya malengo ya mradi huo ni pamoja na kufanya utambuzi na uchunguzi wa hali ya ulemavu ili kubaini mahitaji ya ujifunzaji kwa watoto husika,kuhamasisha uandikishaji wa watoto wenye ulemavu watakaobainika na kupimwa kwenye vituo vya upimaji wa kubaini mahitaji maalumu ya ujifunzaji,kuimarisha ujuzi kazi kwa walimu ili wawe na mbinu za kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu kuweza kujifunza katika madarasa jumuishi na kuboresha miundombinu ya shule za mradi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bi Ester Msoka ambaye Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Misungwi amesema kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na Wadau mbalimbali wa Elimu kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kuboresha huduma ambazo zinatolewa kwa watoto wenye mahitaji maalumu na kutoa wito kwa wadau wengine waendelee kutoa huduma maeneo mengine.
Sambamba na hilo ameongeza kuwa si watoto tu bali hata watu wazima wenye ulemavu wanapewa vipaumbele katika Nyanja tofauti ikiwemo kiuchumi na kijamii pamoja na miundombinu na kuwaomba wadau waendelee kutoa ushirikiano katika Sekta mbalimbali za maendeleo.
Wakati huo huo Diwani wa Kata ya Mabuki Mhe.Petro Lutonja ameshukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuleta mradi wa Elimu Jumuishi wenye thamani Shilingi Milioni 15 katika Kata ya Mabuki ambapo fedha hizo zimeweza kukarabati vyumba 7 vya madarasa pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo.
Mhe. Lutonja ametoa wito kwa Wannachi kuwa pindi Mradi wa Maji utakapofika kutoka Ihelele kwenda Misasi hadi Mabuki,Wananchi watoe ushirikiano wa kutosha na hakutakuwa na fidia kwenye njia zitakapopita bomba ili kurahisisha kupata huduma ya maji kwa Wananchi wa Mabuki.
Naye Mwanafuzi wa Shule ya Msingi Mabuki Bi. Rehema John ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuleta mradi wa maendeleo Ujenzi wa matundu ya vyoo na ukarabati wa madarasa katika Shule ya Msingi Mabuki na kuahidi kutunza vizuri miundombinu iliyojengwa kupitia mradi wa elimu jumuishi katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Mkurugenzi wa SENSE International Tanzania Bi.Naomi Lugoe akiongea na Wadau mbalimbali wa Elimu jana wakati wa kukabidhi ukarabati wa vyumba 7 vya madarasa pamoja na ujenzi wa matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Mabuki.
Baadhi ya Wadau wa Elimu wakisikiliza na kupokea maoni ya Wataalamu kutoka TAMISEMI jana wakati hafla fupi ya kukabidhi ukarabati wa majengo ya madarasa na vyoo katika Shule ya Msingi Mabuki.
Mwonekano wa Vyoo vipya ambavyo vimejengwa kupitia Mradi wa Elimu jumuishi na Shirika la Sense Internatinal katika Shule ya Msingi Mabuki.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.