Wananchi wa Kata ya Misungwi, katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza wajitokeza katika Uzinduzi wa uchimbaji wa msingi wa ujenzi wa vyumba vya Madarasa 20 katika Shule tatu za Sekondari zilizopo katika Kata hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bi. Leokadia Humera amesema kwamba Halmashauri hiyo imepokea fedha cha kiasi cha shilingi Billioni 2.9 kwa ajili ya kutekeleza Miradi ya vyumba 146 katika shule za Sekondari 32 za Serikali zilizopo katika Halmashauri hiyo ambayo ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa zaidi ya vyumba vya madarasa 150 katika shule za Sekondari pamoja na shilingi milioni 90 za kujenga Nyumba ya mtumishi (three in one) katika Kituo cha kutolea huduma za Afya kimoja ambapo tayari maandalizi yameshafanyika katika maeneo yote ya ujenzi ikiwemo kupata mafundi, maandalizi ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi.
Bi. Leokadia Humera ameeleza kwamba Halmashauri ya Misungwi kupitia uongozi na Menejimenti kwa ujumla imejidhatiti kikamilifu na kujipanga kutekeleza na kusimamia miradi hii kwa ubora na uimara na kuwataka Wananchi waendelee kuhamasika na kuiunga mkono Serikali ya awamu ya sita kwa kujitokeza katika kushiriki ujenzi kwa pamoja na lengo ni kuweza kubakisha chenji ambayo itatumika katika kutekeleza mambo mengine ikiwa ni pamoja na kujenga matundu ya vyoo.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ameongeza kuwa Wananchi wamehamasika kuchimba msingi wa ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa ajili ya watoto wao na kwamba anataoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha hizo ambazo katika Halmashauri ya Misungwi zitapunguza tatizo la mrundikano wa Wanafuzni madarasani.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Misungwi Bw. Ananias Mbandwa ameeleza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuwapatia vyumba vya madarasa nane ambapo katika shule hiyo kulikuwa na upungufu wa vyumba kumi na viwili na kwa sasa baada ya madarasa kukamilika utasaidia na kuwezesha Wanafunzi kusoma kwa bidii na kuhamasisha wazazi kusomesha watoto katika shule za Serikali kutokana na ubora utakaokuwepo.
Baadhi ya Wazazi walioshiriki katika uzinduzi huo wa kuchimba misingi katika shule za Sekondari tatu za Kata ya Misungwi wamesema kwamba wamefarijika na jitihada za Serikali za kuweza kuwajengea watoto wao madarasa ili waweze kusoma vizuri na kuipongeza Serikali ya awamu ya sita na kuahidi kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Shule zilizocanza kuchimba misingi katika Kata ya Misungwi ni pamoja na Aime Milembe Sekondari vyumba vya maadarasa sita, Jitihada Sekondari vyumba sita na Sekondari ya Misungwi yenye jumla ya vyumba vya madarasa 8.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.