Watahiniwa 7,879 wanatarajiwa kufanya Mitihani ya kumaliza Elimu ya Msingi mwaka 2020 katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Afisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Bw, Frank Magabiro ameeleza haya ofisini kwake mapema wiki hii, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kisena Mabuba, alisema kwamba Halmashauri hiyo imeshakamilisha maandalizi ya zoezi la kitaifa la uendeshaji wa Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi kwa Wanafunzi wa darasa la saba mwaka 2020.
Afisa Elimu Magabiro amesema kwamba kuna jumla ya Watahiniwa 7,879 waliosajiliwa na wapo tayari kwa ajili ya kufanya Mtihani huo wa kumaliza Elimu ya msingi itakayofanyika kwa siku mbili mfululizo ambapo miongoni mwao Wavulani ni 3,740 na Wasichana ni 4,157 na tayari maandalizi ya msingi yapo vizuri hususani suala la usafiri na usambazaji wa Mitihani kuelekea katika vituo 146 yamekamilika .
Bw, Magabiro alifafanua kuwa kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania inaeleza kwamba Mitihani hiyo ya kumaliza Elimu ya Msingi itaanza siku ya Jumatano tarehe 7 mwezi oktoba mwaka 2020 kuanzia saa 2.00 asubuhi kwa watahiniwa wote kufanya masomo ya Kiswahili , Hisabati na Sayansi na mitihani hiyo itakamilika siku ya Alhamisi ambapo watafanya masomo ya English Language na Maarifa ya jamii.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya Wanafunzi katika masomo, Bw, Magabiro alisema kwamba Wanafunzi wote wameendaliwa vizuri kimasomo ambapo mada zote zilifundishwa vizuri na kukamilishwa, na wamefanya majaribio ya kutosha pamoja na Mitihani mbalimbali ya ngazi ya Kata, Wilaya ukiwemo na Mtihani wa MOCK Mkoa, pia wamejengwa vizuri kisaikolojia na Walimu pamoja na Wazazi ‘’alibainisha kwamba kimsingi Watahiniwa wote wapo vizuri kwa ajili ya kufanya Mitihani hiyo’’. Alisisitiza Bw, Magabiro.
Afisa Elimu huyo ameongeza kuwa kwa upande wa Watahiniwa wa Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi mwaka huu 2020 kumekuwepo na ongezeko la Watahiniwa 87 ukilinganisha na Watahiniwa 7,792 waliohitimu Elimu ya Msingi mwaka 2019 katika Halmashauri ya Misungwi.
Bw, Frank Magabiro ameeleza kwamba baadhi ya sababu iliyowezesha kuongezeka kwa Watahiniwa hao ni pamoja na udhibiti wa utoro kwa Wanafunzi, mwitikio wa Wazazi na jamii katika suala la Elimu sambamba na utekelezaji wa Sera ya Serikali ya utoaji wa Elimu bila malipo ambayo inatekelezwa katika Shule zote za msingi 147, zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi zikwemo Shule za Serikali 139 na shule binafsi 8.
Baadhi ya Wasimamizi na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Wilayani Misungwi wakiwa katika Semina maalum ya maandalizi ya Mitihani ya darasa la saba mwak 2020 katika Ukumbi wa Shule maalum ya Mitindo hivi karibuni.
Amewataka Watahiniwa hao kufanya mitihani yao katika hali ya amani na kuwa watulivu na kutambua kwamba Mtihani huo wa Taifa ni sawa na Mitihani mingine na kuwatakia afya njema wakati wote na kuwaomba wamtangulize Mungu awasaidie, sambamba na kuwaomba wasimamizi wa Mitihani kusimamia vizuri mitihani hiyo kulingana na maelekezo na taratibu zilizotolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania.
Afisa Elimu Msingi Wilaya ya Misungwi, Frank Magabiro akiwa ofisini kwake kwa ajili ya maandalizi maalum ya zoezi la Mitihani ya darasa la saba mwaka 2020.
Viongozi na Maafisa Elimu wa ngazi ya Mkoa na Wilaya wakiendelea na utoaji wa maelekezo mbalimbali katika semina maalum ya maandalizi ya Mitihani ya darasa la saba mwaka 2020 kwa Wasimamizi na Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Wilayani Misungwi.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.