Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Veronica Kessy atembelea na kukagua maeneo ya wachimbaji wa Madini na kuwahakikishia ushirikiano na Serikali kutatua changamoto zinazowakabili Wachimbaji Wilayani humo.
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Veronica Kessy amewataka Wachimbaji hao kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kushughulikia na kutatua changamoto na kero mbalimbali zinazowakabili zikiwemo ukosefu wa maji, umeme na ubovu wa barabara na kuwataka waendelee kuchapa kazi na kuongeza mapato ya Halmashauri na kukuza uchumi taifa.
Mkuu wa Wilaya hiyo ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa katika ziara yake pamoja na Wajumbe wa Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya katika Machimbo ya Mwanangwa, Shilalo, Mwamazengo na Ishokela na kusisitiza kwamba Serikali ipo na inatambua changamoto zao na wanaendelea kuzishughulikia ambapo kwa upande wa barabara watawasiliana na TARURA kuona mpango wa Bajeti ya fedha au kuomba maombi maalum ya matengenezo ya barabara ya Shilalo na Mwamazengo, pia suala la umeme na Wilaya ya Misungwi ni vijiji 42 tu vilivyobaki kuwekewa umeme kati ya Vijiji 114 na tayari Mkandarasi wa umeme anaendelea kufanya maandalizi.
Mhe, Veronica Kessy alieleza kwamba katika changamoto ya maji katika maeneo ya Machimbo hayo na kuwahakikishia kwamba mpango wa kuweka maji ya kutosha katika machimbo hayo ya Mwamazengo pamoja na Shilal utafanyiwa kazi pamoja na kuzitatua kwa kuunganishwa na maji kutoka katika chanzo cha KASHWASA – Ihelele kupitia mpango wa Wakala wa Maji vijijini (RUWASA)
Mkuu wa Wilaya huyo amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Misungwi kufuatilia suala la utunzaji na uhifadhi wa mazingira pamoja na mambo ya ardhi ambapo changamoto hiyo ilijitokeza katika machimbo ya Shilalo kwa mchimbaji mmoja kubainisha kwamba Serikali iweke mkakati wa kutenga maeneo ya makaburi na kuimarisha utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya sasa na baadae
Mmoja wa Wachimbaji wa Kikundi cha Mlimani Group Machimbo ya Shilalo Jeremiah Kitundu amesema kwamba kero waliyonayo ni tatizo la barabara kuelekea katika machimbo ya Shilalo na tatizo la maji na umeme ambapo suala la maji limetatuliwa na Serikali lakini bei ni kubwa na yanatoka mara moja kwa wiki, ambapo maji yanatumika katika uchenjuaji wa dhahabu sambamba na changamoto hizo machimbo hayo yameweza kuongeza mapato ya Serikali na tayari Machimbo hayo tangu yaanze yamechangia fedha nyingi kwa Serikali.
Mchimbaji mwingine wa Machimbo ya Mwamazengo Mrisho Masebu ameeleza kwamba kwa upande wake amesaidia sana katika shughuli za Serikali ikiwemo na ujenzi wa Shule , madawati na wameweza kuchangia mapato ya Halmashauri tangu mwaka 2015, na kuomba Serikali iweze kupeleka maji na umeme katika machimbo hayo ya Mwamazengo.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Veronica Kessy (katikati) akiwa katika kikao cha pamoja na Viongozi wa Kata na Kijiji cha Shilalo na baadhi ya Wawakilishi wa Wachimbaji wadogo wa Madini ya Dhahabu wenye Leseni kwa ajili ya kuzungumza matatizo yanayowakabili Wachimbaji hao (kushoto ni) Petro Sabatto Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Shilalo.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.