Shirika la Amani Girls Home la Mwanza latarajia kuanza utekelezaji wa mradi wa AMKA katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa lengo la kuboresha lishe kwa Watoto na akina mama wajawazito mwaka huu 2020.
Hayo yamebainishwa na Mratibu wa Shirika la Amani Girls Home, Revocutus Sono wakati wa kikao cha kutambulisha mradi huo kilichofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Graceland kilichowahusisha Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi pamoja na Wataalam wa Shirika hilo.
Bw, Sono ameeleza kuwa mradi huo utatekelezwa mwanzoni kwa majaribio katika Kata nane (8) za Halmashauri hiyo kwa gharama ya shilingi millioni 65 kwa lengo la kuboresha lishe kwa Watoto chini ya umri wa miaka mitano pamoja na akina mama walio kwenye umri wa uzazi, na lengo la mradi huu ni kutekelezwa katika Vijiji vyote 114 vya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Amefafanua zaidi kwamba mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano na Wadau wengine wakiwemo Shirika la PANITA ambalo ni Jukwaa la Lishe Tanzania kwa pamoja katika kuhamasisha Wananchi vijijini kuhusu umuhimu wa masuala ya Lishe bora kwa Watoto wenye umri mdogo sambamba na akina mama wenye umri wa uzazi ili kuweza kuboresha Afya zao.
Mwenyekiti wa kikao hicho Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi, Bw, Peter Sabatto akifunga kikao hicho amewataka Wadau wa maendeleo kushirikiana kwa pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi katika kutekeleza masuala ya Lishe kwa Wananchi na kuwahakikishia amani na usalama wakati wote wa utekelezaji wa mradi huo, na kwamba Serikali inatambua juhudi za Wadau na Wafadhili mbalimbali wanaoendelea kusaidia maendeleo katika sekta zote kwa lengo la kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020.
Peter Sabato Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi akisisitiza jambo kuhusu umuhimu wa Lishe kwa Wananchi wa Wilaya ya Misungwi, kwenye kikao cha Wadau katika Ukumbi wa Hoteli ya Graceland
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Bw, Kisena Mabuba amewataka Wataalam na Maafisa Ugani wa Idara ya Kilimo na Mifugo kupitia mpango wa Kitaifa wa Lishe na kuweza kutoa elimu kwa Maafisa waliopo katika ngazi za chini ili kuwawezesha kuhamasisha na kuhimiza Wananchi katika masuala ya lishe pamoja na kusisitiza kilimo cha mazao muhimu ya chakula na ufugaji wa mifugo ikiwemo kuku wa mayai.
Bw, Kisena Mabuba amesema kwamba ni muhimu sana Wananchi wapewe elimu na kujengewa uelewa wa masuala ya lishe na kuweza kuendeleza kwa baadae hii ni kutokana na Sera na mwelekeo wa Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa kujitegemea na kupunguza ufadhili unaotolewa kwa masharti mbalimbali yasiyokuwa na tija na taifa.
Baadhi ya Washiriki wa kikao cha Viongozi kwa ajili ya kutambulisha mradi wa AMKA wakisikiliza mada kwa lengo la utekelezaji mradi wa Lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.