Serikali Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza imepiga marufuku vitendo vya Walimu kuwatumikisha Wanafunzi kwenye shughuli za mashamba yao binafsi na majumbani hivyo kusababisha kuzorota kwa elimu.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda wakati wa ziara ya kukagua Miradi na shughuli za maendeleo iliyofanyika katika Kata ya Gulumungu Tarafa ya Inonelwa Wilayani humo kwa lengo la kutembelea na kuona utekelezaji wa miradi katika Zahanati ya Nyamayinza, Shule ya Sekondari J. Magufuli na Shule ya Msingi Mwakiteleja, Miundombinu ya barabara na Maji pamoja na miradi ya sekta zingine.
Akizungumza na Viongozi, Wananchi na Walimu katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya maeneo ya Shule ya Sekondari J. Magufuli Kijiji cha Nyamayinza Kata ya Gulumungu, baada ya kusikiliza kero na malalamiko ya Wananchi hao Mkuu wa Wilaya huyo, amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya Walimu ambao wanaendelea kuwatumikisha pamoja na kuchapa viboko Wanafunzi bila utaratibu maalum na kusababisha migongano baina ya Walimu hao na Wazazi pamoja na kuzorotesha utoaji wa elimu bora hatimaye kusababisha kushuka kwa kiwango cha taaluma na ufaulu.
“ Ninyi Walimu nataka niwaambieni mzingatie maadili ya taaluma yenu, kazi kubwa kwenu nikufundisha, hivyo ni marufuku kuanzia leo kwa Wanafunzi hawa kulima katika mashamba yenu binafsi pamoja na kuwapa kazi majumbani mwenu, pia nawataka mtekeleze na kusimamia haya ambapo mashamba ya shule yabaki kutumiwa na shule yenyewe kwa ajili ya kulima mazao ya Chakula na siyo Walimu kujinufaisha nayo tena,”alisititiza na kuagiza Mkuu wa Wilaya Juma Sweda.
Juma Sweda, amewataka Viongozi wa Vijiji na Kata zote Wilayani humo kusimamia kikamilifu maendeleo ya utoaji wa elimu na taaluma na kuhakikisha uadilifu na nidhamu kwa Walimu na Wanafunzi unadumishwa pamoja na kuendelea na utoaji wa chakula na masomo ya ziada kwa Wanafunzi ili kuboresha na kuongeza kiwango cha taaluma na ufaulu wa Wanafunzi na kutimiza mpango mkakati wa Wilaya wa kuondoa “Division Four na Ziro” kwa mwaka 2020.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda (kulia) akisalimiana na kumuuliza maswali kuhusu masomo Mwanafunzi wa Kidato cha Pili katika Shule ya Sekondari J.Magufuli wakati wa ukaguzi wa madarasa na kuona maendeleo ya Wanafunzi wa shule hiyo uliofanyika katika ziara aliyoifanya hivi karibuni.
Mmoja wa Wakazi wa Kijiji cha Nyamayinza akitoa kero na malalamiko yake kwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, kuhusu adhabu wanayopatiwa Wazazi wanaozesha na kuwapa mimba watoto wa shule.
Mkuu wa Wilaya huyo pia amewaagiza Viongozi hao pia kuwasaka watoto watatu (3) ambao hawajaripoti kidato cha kwanza mpaka sasa katika Sekondari ya J. Magufuli , kuhakikisha wanapatikana na wanaanza masomo haraka, vile vile amekemea tabia ya baadhi ya Wazazi wanaowaozesha na kuwapa mimba watoto wa shule na kukatisha ndoto zao na kuwaonya waache tabia hiyo chafu vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao hatimaye kufungwa maisha.
Ameongeza kwamba ni vyema Viongozi wa nagzi za Vijiji na Vitongoji kutambua nafasi na wajibu wao katika kutekeleza majukumu ya Serikali na kuleta maendeleo kwa Wananchi pamoja na kuhakikisha wanatunza na kulinda amani na usalama katika maeneo yao hususan katika kipindi hiki cha maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020, hivyo wanapaswa kuimarisha ulinzi wa Jeshi la jadi la Sungusungu.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Kata ya Gulumungu, Valentine Lukandiza amesema kwamba amepokea maagizo na maelekezo yote yaliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, na watahakikisha wanatekeleza na kusimamia masuala ya kuboresha taaluma katika shule za Msingi na Sekondari kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria zilizopo ili kuweza kutatua kero na kuwaletea maendeleo Wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.