Serikali kujenga bweni la shilingi Milioni 75 kwa ajili ya kulala Wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Misungwi, Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza ikiwa ni jitihada za kupunguza na kuondoa tatizo la kutembea umbali mrefu.
Akizungumza na Viongozi na Wanafunzi katika Shule ya Sekondari Misungwi, wakati wa ziara ya kikazi Wilayani Misungwi, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, anaeyeshughulikia Elimu, Gerald Mweli ametoa ahadi ya Serikali kupitia Wizara ya ofisi ya Rais - TAMISEMI kwamba watajenga bweni moja la Wanafunzi kwa gharama ya shilingi Milioni 75 na kueleza kuwa amekagua ujenzi unaoendelea na kuridhishwa na kazi zinazofanyika na tayari Wizara imeshapokea maombi ya fedha za ujenzi wa mabweni.
“ Sisi kama ofisi ya Rais –TAMISEMI kupitia kwa Mhe, Waziri Jaffo alipokea maombi yenu ya ujenzi wa bweni kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, na sisi baada ya kuona juhudi hizi tumeona tutafute fedha, na tutajenga bweni moja ambapo hali na uwezo ukiruhusu tutaongeza bweni lingine,”alifafanua kwa msisitizo zaidi Naibu Katibu Mkuu, Mweli.
Naibu Katibu Mkuu huyo, amewapongeza Viongozi na Watendaji wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa kusimamia vizuri maendeleo ya sekta ya elimu pamoja na jitihada za kupunguza mdondoko wa Wanafunzi katika elimu, sambamba na suala la kuwachukulia hatua za kinidhamu baadhi ya Walimu wasiozingatia na kufuata maadili ya ualimu na kuongeza kiwango cha ufaulu katika matokeo ya darasa la saba, kidato cha Nne na sita mwaka jana 2019.
Bw, Mweli amempongeza Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Misungwi, Ananias Mbandwa kwa kazi nzuri aliyoifanya na kuweza kuokoa fedha zaidi ya Milioni 30 zilizotolewa na Serikali za ununuzi wa Chakula na kununua kwa bei ya sokoni, ambazo ameamua kuanzisha ujenzi wa bweni la Wasichana ambalo linaendelea kujengwa, amesema kwamba, hii ndo aina ya viongozi tunaowataka, viongozi wanaoishi ndani ya changamoto na wanashiriki katika kutatua changamoto na wanasherekea mafanikio kwa pamoja.
Wakati huo huo, baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Misungwi, akiwemo kaka Mkuu wa Shule hiyo, Timoth John anayesoma kidato cha Nne pamoja na Dada Mkuu Yustina Antipas ambaye ni Mwanafunzi wa kidato cha Tano kwa nyakati tofauti wametoa salamu za pongezi na shukrani kwa Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, John Pombe Joseph Magufuli kwa juhudi kubwa aliyowafanyia Watanzania kwa kutoa elimu bila malipo, ambapo utaratibu huo umeongeza idadi ya Wanafunzi na kupunguza Watoto wa mitaani na wanaoishi katika mazingira magumu hatimaye kiwango cha ufaulu kimeongezeka.
Wanafunzi hao wamebainisha mikakati yao pamoja na Walimu kwa mwaka huu 2020 ambayo ni kuhakikisha wanaondoa ufaulu wa daraja sifuri katika matokeo ya kidato cha Nne, sambamba na kufuta ufaulu wa daraja la nne, na daraja la tatu katika matokeo ya kidato cha sita, na wameweza kuahidi kuweka historia na mapinduzi makubwa katika ufaulu wa mitihani ya mwaka 2020.
Katika ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu -TAMISEMI Wilayani hapa, ameweza kukagua na kuona shughuli za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Jengo la bweni la Wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari ya Misungwi, kutembelea na kuzungumza na Wanafunzi wa shule ya msingi maalum ya Mitindo pamoja na kuzindua zoezi la kitaifa la ugawaji wa Vitabu vya kiada vya kufundishia Wanafunzi wa darasa la sita katika masomo yote, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imepata vitabu zaidi ya elfu 26.
Jengo la bweni la Wasichana linaloendelea kujengwa katika Shule ya Sekondari Misungwi ambalo litagharimu shilingi Milioni 110 hadi kukamilika., ujenzi huu ulianza kwa fedha shilingi milioni 30 ambazo ziliokolewa na Mkuu wa Shule hiyo Mwl, Ananias Mbandwa na baadaye Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia kutoa fedha za kukamilisha ujenzi huo mwaka 2020.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kisena Mabuba (katikati) akitoa taarifa ya maendeleo ya shughuli za Sekta ya Elimu kwa mawaka 2019/2020 kwa Naibu Katibu Mkuu - TAMISEMI, Gerald Mweli wakati wa ziara ya kikazi ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji Wilayani Misungwi mapema jana, (kulia) ni Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Misungwi, Diana Kuboja akifuatilia kwa makini.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.