Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe, Mhandisi Robert Gabriel aridhishwa na kupongeza utendaji wa Baraza la Madiwani na Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza
Mkuu wa Mkoa Robert Gabriel alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo liloketi kwa ajili ya kupitia na kujadili taarifa ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo.
Mhandisi Robert Gabriel amesema kwamba ameridhishwa sana na utendaji wa Madiwani na Watendaji wa Halmashauri ya Misumgwi ambapo kutokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2019/2020 imeonyesha kuwa hoja ni chache na baadhi yake ni za kawaida na dhahiri kwamba usimamizi wa matumizi ya fedha za umma unaridhisha na katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo inatekekelezwa kikamilifu pamoja na suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mhandisi Gabriel amewataka Watendaji kuongeza ushirikiano kwa kufanya kazi kama timu na kwa kufanya hivyo kutasababisha na kufanya mambo mambo mengi makubwa na ya ajabu na kuongeza mafanikio makubwa zaidi katika maendeleo ya miradi kwa Wananchi, na kuwataka Watendaji kuendelea kujibu Hoja vizuri na kuendelea kufanya matumizi ya fedha kwa kuzingatia kanuni, taratibu na sheria za fedha ili kuepuka hoja zisizokuwa za msingi.
Awali akiwasilisha taarifa ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2019/2020 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kisena Mabuba amesema kwamba katika ukaguzi huo Halmashauri hiyo imepata Hati ya Kuridhisha (Hati safi) ambapo hoja zilizohojiwa kwa mwaka 2019/2020 zinaendelea kutekelezwa ambazo ni pamoja na Hoja 8 zilizotekelezwa, Hoja 19 zinazoeendelea kutekelezwa na kufanya kuwa na Hoja 27 kwa mwaka huo.
Kisena Mabuba ameeleza kwamba kulikuwapo pia Hoja za nyuma ambazo ni 18 ambapo Hoja 16 zinaendelea kutekelezwa na Hoja 2 ambazo hazijatekelezwa na kuwa na idadi ya jumla ya Hoja 45 zilizohojiwa, na Menejimenti inaendelea kufuatilia hoja hizo na kuzitekeleza na baaadae kuhakikiwa na Wakaguzi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mhe, Kashinje Machibya ameeleza kuwa kwa ujumla Baraza la Madiwani limeendelea kusimamia kikamilifu shughuli za maendeleo ikiwemo miradi, Ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri, utendaji kazi wa Watendaji ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji na kuchukua hatua za kinidhamu mara inapobainika pamefanyika kinyume na sharia, kanuni na taratibu.
Mhe, Machibya amesema kwamba kutokana na usimamizi mzuri wa Baraza la Madiwani ndio umeleta mafanikio ambapo katika ukaguzi huo zimeonekana hoja chache ambazo ni nyepesi za kiutendaji zaidi na kuahidi kuendelea kusimamia kikamilifu utendaji ili katika ukaguzi ujao kuwa na hoja chache na zilizo na majibu yanayotosheleza.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wialaya ya Misungwi, Mhe, Kashinje Machibya akizungumza na kutoa Salaam katika Mkutano maalum wa Baraza la Madiwani la Halmashauri la kujadili Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali akiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza ,Mhandisi Robert Gabriel (kulia) pamoja na Viongozi wengine wa Wilaya ya Misungwi.
Baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wa Baraza la Halmashauri ya WIlaya ya Misungwi wakifuatilia mjadala wa Mkutao kwa makini wakati Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel akitoa maelekezo kwa Madini na Watendaji wa Halmashauri hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.