Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka na kuwakumbusha wazee kuendelea kushirikiana na serikali katika kuelimisha vijana kuwa na Maadili mema na kuachana na tabia hasi zinazosababisha kuwepo na mmomonyoko wa Maadili Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo tarehe 07, Juni, 2024 wakati akizungumza na wazee wa wilaya ambao kwa kauli moja wameonesha imani kubwa kwa Rais Samia katika kuliletea Taifa maendeleo.
"Ni lazima tujenge familia bora na imara, tunapaswa kujiandaa na kustaafu mapema na sio kuongeza mke bali tunapaswa kujiandaa na uzee kwa kujiandalia mahali pa kuishi." Mhe. Mtanda.
Amebainisha kuwa fidia zinazolipwa kwa wananchi wa Fela wanaopisha mradi wa SGR ni ishara ya hatua kubwa zaidi ya maendeleo inayokuja kwa wananchi wa
Misungwi hivyo ni lazima kujiandaa kunufaika nazo kwa kuwekeza.
"Mradi wa kimkakati wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 700 (Daraja la Kigongo Busisi) unakaribia kukamilika, ndani ya miezi 3 daraja letu linakamilika na kupitia takwimu za abiria wanaotumia kivuko inaonesha kuna watu wengi sana wanatumia barabara hiyo, tujiandae kunufaika," Amesisitiza Mkuu wa Mkoa.
Vilevile, ameutaja mradi wa Ujazilizi wa Umeme wenye thamani ya zaidi ya Bilioni 8 na kuna megawati za umeme zaidi ya 80 lakini unaotumika ni umeme kidogo tu na kwamba zaidi ya Bilioni 11 zimekuja kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme (REA).
"Serikali inasisitiza malezi bora ya watoto kuanzia unyonyeshaji hadi makuzi na kuwapatia elimu bora ili baadaye waweze kuwatunza wazee wao na serikali inawahakikishia usalama popote walipo hata walio kwenye vituo vya malezi maalum na wafufaika wa mradi wa Uhaulishaji fedha chini ya TASAF wataendelea kunufaika kwa mujibu wa taratibu." Mtanda.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Misungi Mhe. Johari Samizi amesema tatizo la Maji kwenye kata ya Usagara linakwenda kumalizika hivi karibuni kwani tayari kuna mkandarasi anayejenga mradi wa Maji mkubwa kwenye kata hiyo yenye vijiji vinne na akatoa agizo kwa watumishi wa Afya kuwajali wazee bila kuchoka.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wilaya ya Misungwi Josiah Gambishi amesema anajivunia umoja na ushirikiano walionao ndani ya wilaya hiyo unaochagizwa na uongozi bora wa Mkuu wa Wilaya hiyo na kwa kauli moja wameonesha imani kwa uongozi wa Rais Samia na kusema anatosha kuongoza nchi kwa miaka 5 mingine.
Baadhi ya Wazee wakifuatilia na kusikiliza Hutoba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.Said Mtanda jana katika ukumbi wa MGS wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya maendelea Wilayani Misungwi
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.