Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe, Adam Malima azindua vyumba 44 vya madarasa yenye thamani ya shilingi milioni 880 katika Halmashauri ya Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Amezindua vyumba hivyo 44 vya madarasa mwishoni mwa wiki katika Shule ya Sekondari Idetemya ambayo imekamilisha ujenzi wa vyumba 6 vya madarasa kwa gharama ya shilingi 120,000,000 ambapo Halmashauri imeweza kujenga vyumba vyote 44 vya madarasa katika shule 15 za Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Mhe, Adam Malima ametoa rai kwa Viongozi wa Halmashauri hiyo kuweka juhudi za kuongeza eneo kwenye shule mpya ya Jitihada iliyopo katika Kata ya Misungwi ili kusaidia shule hiyo kuwa na uwezo wa kupanuka kwa kuongeza miundombinu mingine ikiwemo ya Viwanja vya michezo pamoja na madarasa kutokana na shule hiyo kuwa katika maeneo ya mjini yenye ongezeko kubwa la idadi ya watu.
"Hamuwezi kuwa na shule mpya leo hii yenye hekari sita pekee, fanyeni jitihada kuongeza eneo ili kuiwezesha kumudu ongezeko la wanafunzi kwa mipango ya sasa na baadae na msitegemee kuanzisha shule mpya mbali kwani zitakua na gharama ya usafiri kwa wazazi katika kuhakikisha watoto wao wanafika shuleni",Amesisitiza Mhe, Malima.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amewapongeza na kuwapa Kongole Viongozi wa Halmashauri hiyo kwa usimamizi mzuri na kuhakikisha eneo la shule linapandwa Miti ya kutosha na kuomba Halmashauri zingine Mkoani humo kuiga mfano wa Halmashauri ya Misungwi na Magu ambazo zimekuwa mfano bora katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira kitendo ambacho kitarejesha uoto wa asili na kuondoa hewa ya ukaa.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Ndugu Balandya Elikana amewataka wazazi na walezi wote Wilayani Misungwi kuhakikisha wanawapeleka watoto shule kuanza kidato cha kwanza kutokana na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ameshajenga madarasa na miundombinu mingine pamoja na kuweka madawati , viti na meza ili watoto waweze kusoma vizuri .
Awali katika uwasilishaji wa taarifa ya ujenzi vyumba 44 vya madarasa ilibainishwa kwamba ujenzi wa vyumba hivyo vya madarasa umefanyika sambamba na matengenezo ya Samani kwa wanafunzi ambapo Seti za viti na meza 1,760 zimetengenezwa ambazo zitanufaisha wanafunzi 1, 767 wa kidato cha kwanza kwa mwaka 2023.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe,Veronika Kessy ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa madarasa 44 ambazo kwa Wilaya ya Misungwi zimesaidia kupunguza changamoto ya umbali wa baadhi ya Wanafunzi kutoka shule moja hadi nyingine, na kwamba atahakikisha wazazi na walezi wanapeleka watoto kuanza kidato cha kwanza mapema pamoja na kusimamia utunzaji wa miundombinu ya madarasa ili yaweze kuleta tija na manufaa yaliyokusudiwa na kudumu kwa muda mrefu.
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza,
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.