Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Juma Sweda awataka na kuwasihi Wananchi kujitokeza kumpokea Mhe, Samia Suluhu Hassan Rais wa Jmhuri ya Muungano wa Tanzania katika ziara yake ya kikazi Wilayani Misungwi tarehe 14 mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa Habari ofisini kwake Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda amesema kwamba Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan atakuwa na ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Misumgwi siku ya jumatatu tarehe 14 mwezi Juni ambapo atatembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Daraja la Magufuli katika maeneo ya Kigongo – Busisi.
Juma Sweda amesema katika ziara hiyo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Samia Suluhu Hassan katika Wilaya ya Misungwi atafanya Uzinduzi wa Mradi Mkubwa wa Maji wa Nyahiti – Misungwi uliojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 12 ambao utanufaisha Wananchi wa Kata ya Misungwi na Igokelo pamoja na kuweka Jiwe la msingi katika ujenzi wa mradi wa Reli ya kisasa (SGR) eneo la Fella.
Mhe. Juma Sweda amewataka Wananchi wote kutoka maeneo ya Wilaya ya Misungwi na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kumpokea na kumlaki Mhe, Rais katika maeneo yote ya miradi atakapotembelea kwa ajili ya shughuli ikiwemo kuzungumza na Wananchi katika eneo la uzinduzi wa mradi wa maji wa Nyahiti – Misungwi katika tanki la maji la Bomani Masawe na eneo la uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa Reli ya kisasa SGR Fella.
Amewataka na kuwaomba Wananchi pamoja na Wafanyafabiashara ndogo ndogo kujitokeza na kutumia fursa hiyo kwa ajili ya kuweza kutoa huduma na kuuza bidhaa za chakula kwa Wananchi watakaokuwepo maeneo hayo ili pia kuweza kushuhudia na kumsikiliza Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na kuona miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya awamu ya sita.
Wakati huo huo, katika taarifa yake Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Misungwi ameeleza kwamba katika ziara hiyo ambayo itahudhuriwa na Viongozi wengine wa Chama na Serikali, ngazi ya Taifa , Mkoa na Wilaya pia kutakuwepo na Vikundi mbalimbali vya burudani za ngoma za Asili, Kwaya, na Wasanii wa Tanzania akiwemo Peter Msechu, Harmozer na wengine wengi watakaotoa burudani kabambe wakati wa shughuli nzima katika maeneo ya miradi husika.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.