Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Misungwi, Jamali Babu na Viongozi wengine wa CCM wakihakiki kura za mgombea Ubunge Alexander Mnyeti aliyepata kura 406 huku mgombea mwenyewe akishuhudia kura hizo.kwa karibu.
Mmoja wa Wagombea wa Ubunge Jimbo la Misungwi, Alexander Mnyeti (katikati) akionyesha karatasi yenye namba yake 29 kwa wapiga kura za maoni katika Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Misungwi mapema leo.
Wajumbe 406 wa Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Misungwi wamchagua Alexander Mnyeti katika Uchaguzi wa kura za maoni kuwa mgombea wa nafasi ya Ubunge kuwakilisha Jimbo la Misungwi, Mkoani Mwanza katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Msimamizi wa Uchaguzi Wilaya ya Misungwi, Jamal Babuu amemtangaza Alexander Mnyeti kuwa ameongoza kwa kupata jumla ya kura 406 kati ya kura 791 ya kura zote zilizopigwa na Wajumbe wa Mkutano huo, ambapo kura halali zilizopigwa ni 786 na kura 5 ziliharibika, huku wagombea wachache 42 wakipata kura zilzosalia na wengine wakiambulia kura sifuri.
Amesema kwamba Uchaguzi huo ulikuwa wa huru na haki na awali wagombea wote 45 walipewa nafasi sawa ya kujinadi na kueleza sera na mikakati yao mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu na baadae kura za wazi zikapigwa na kuhesabiwa hadharani na kushuhudiwa na wagombea wote.
Jamali Babu ameeleza kuwa Charles Kitwanga amepata kura 260 na kushika nafasi ya pili ambapo Chanila David Mwakyoma akipata kura 59 na kuwa katika nafasi ya tatu kati ya wagombea wote 45 waliojitokeza kuwania nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Misungwi kupitia tikiti ya Chama cha Mapinduzi mwaka huu 2020.
Amewataka wagombea na wajumbe wote kuwa wamoja na kuvunja makundi na kuendelea kusaidia chama ili kuweza kupata ushindi mzuri katika Uchaguzi ujao kwa kumuunga mkono mgombea atakayeteuliwa na ngazi za juu za Chama cha Mapinduzi kwa mujibu wa utaratibu na kanuni zilizowekwa kutokana na kwamba Mkutano Mkuu wa Wilaya siyo wa mwisho katika mchakato mzima wa kura za maoni ndani ya chama, na kuwashukuru wajumbe kwa kutumia haki yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Misungwi, Daud Gambadu amewashukuru na kuwapongeza wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa CCM Wilaya ya Misungwi kwa kazi kubwa ya kutenda haki na kutoa maamuzi kwa kuchagua Viongozi wanaowataka na kuwaomba waende kujiandda tena kwa ajili ya Uchaguzi wa kura za maoni za Madiwani kwa ngazi ya Kata zitakazofanyika hivi karibuni, ambapo wanapaswa kutenda haki kwa kuchagua kiongozi bora.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.