Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza, imeanza kutekeleza mpango wa utoaji wa zawadi za vinyago kwa viongozi wa Kata na shule zilizopata ufaulu hafifu katika matokeo ya Mitihani ya taifa ya shule za Msingi na Sekondari ya mwaka 2019, ili kuhamasisha jitihada za ushindani hatimaye kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Akizungumza katika kikao cha Wadau wa Elimu Wilayani Misungwi,kilichofanyika katika Ukumbi wa MGS Misungwi hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kisena Mabuba amesema kwamba katika Elimu suala la Motisha ni la msingi na muhimu sana na tayari utaratibu wa kutoa zawadi umeanzishwa rasmi na ni endelevu ambapo Shule na Kata zitakazokuwa zinafanya vizuri zitapewa zawadi chanya ikiwemo vyeti, ngao, vifaa na fedha taslimu sambamba na kutoa zawadi hasi kwa wale watakaofanya vibaya katika matokeo ikiwa ni pamoja na kupatiwa zawadi ya Vinyago.
Bw, Kisena ameeleza kuwa Halmashauri imeamua na kuweka mkakati na malengo ya kuhakikisha Wanafunzi wa shule za msingi wanafaulu kwa asilimia 100 na wote wanajiunga na Sekondari pamoja na kuongeza ufaulu kwa Wanafunzi wa Sekondari sambamba na kufuta daraja sifuri kwa mwaka huu 2020 na baadae kuondoa ufaulu wa daraja la 4 katika shule zote za Sekondari Wilayani hapa.
Afisa Elimu Sekondari Wilaya, Diana Kuboja amesema kuwa shule za msingi zilizofanikiwa kupata zawadi ya ushindi ni pamoja na shule tatu za Serikali ambazo ni Mwakiyenze, Kwimwa na Ngeleka na shule ya Lwasa English medium inayomilikiwa na mtu binafsi, aidha, kwa upande wa Sekondari, shule zilizofanikiwa kufanya vizuri ni Ipwaga Sekondari inayomilikiwa na mtu binafsi, pamoja na shule ya Serikali ya Sekondari ya Mbarika, zilizofanikiwa kufuta daraja sifuri katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.
Bi, Diana Kuboja amezitaja shule zilizopata ufaulu hafifu na kushika mkia kiwilaya ni, shule ya Sekondari Mawematatu ya Kata ya Mabuki na shule ya msingi Mwamazengo iliyopo Kata ya Lubili katika matokeo ya mitihani ya Taifa ya shule za Sekondari na Msingi mwaka jana, ambapo Kata ya Nhundulu imeshika nafasi ya mwisho kiwilaya
Wakati huo huo, Shule tatu za Serikali kati ya shule ishirini na nane za Sekondari za wilayani humu, zimeibuka kuwa shule bora katika matokeo ya Kidato cha nne mwaka jana Shule hizo ni pamoja na Mbarika Sekondari, Nyabumhanda Sekondari pamoja na Sekondari ya Paulo Bomani, baada ya kupata idadi kubwa ya kiwango cha ufaulu kuanzia daraja la kwanza, daraja la pili na daraja la tatu huku matokeo hayo yakiashiria kiwango cha juu cha ufaulu wilayani hapa,
Bi, Kuboja aliongeza kwamba zawadi zilizotolewa kwa shule bora za Sekondari ni pamoja na vifaa vya maabara vyenye thamani ya shilingi milioni 10 pamoja na fedha taslimu shilingi milioni tatu, wakati shule za msingi zikipatiwa fedha taslimu shilingi milioni moja na laki nne, pamoja na ushindi huo pia shule ya Sekondari Misungwi imeibuka kidedea, baada ya kufuta daraja la nne na daraja sifuri, katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa kidato cha sita mwaka jana.
Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imefanikiwa kushika nafasi ya 3 kimkoa katika ufaulu wa Mtihani wa kidato cha Nne na nafasi ya 90 kitaifa kwa ufaulu wa asilimia 82 sambamba na kupata nafasi ya 5 kimkoa katika ufaulu wa Mtihani wa kumaliza Elimu ya msingi na nafasi ya 117 kitaifa kwa ufaulu wa asilimia 79.6 mwaka jana 2019.
Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ina jumla ya shule za msingi 149 ambapo kati ya hizo shule tisa zinamilikiwa na watu binafsi, huku shule za Sekondari zikiwa 34 ambapo kati ya hizo shule sita zinamilikiwa na watu binafsi.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda (wa tatu kushoto) akikabidhi Zawadi ya Vifaa vya Maabara kwa Viongozi wa Shule ya Sekondari ya Kata ya Mbarika iliyofuta daraja sifuri mwaka 2019, ( wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kisena Mabuba na katikati ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya, Daud Gambadu akifuatiwa na Diwani wa Kata ya Mbarika, Joel Dogani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kisena Mabuba akizungumza na wadau wa Elimu kwa msisitizo kuhusu Viongozi wa Kata na Vijiji kusimamia Elimu mashuleni na kuweka mikakati ya kuongeza ufaulu wa Wanafunzi katika Mitihani yao ya darasa la saba na kidato cha Nne na sita na hatimaye kuondoa na kufuta daraja sifuri na daraja la 4 mwaka huu 2020.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.