Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita imekamilisha mchakato wa manunuzi ya mitambo miwili maalum ya kuopoa magugumaji aina ya Salvinia na Mtambo mkubwa wa kuondoa magugu maji aina ya Lutenda kabla ya Mwisho wa Mwezi Julai 2025.
Ameyasema hayo leo Tarehe 19 Mei 2025 akiwa katika kijiji cha Kigongo Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza akikagua maendeleo ya udhibiti wa magugumaji aina ya Salvinia eneo la Kigongo na Busisi (Ziwa Victoria) Mhe. Majaliwa amewashukuru wananchi na kwa jitihada za awali za kutumia mikono na mitumbwi kuhamisha na kusafisha ziwa ambapo Serikali ina mpango wa kusafisha maeneo yote yanayozunguka ziwa victoria ikiwemo mikoa yote ya Kanda ya Ziwa ili kuhakikisha gugumaji hilo linaondolewa na hali hiyo haitokei tena.
Akisoma taarifa ya magugumaji hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mwenyekiti wa timu ya kuondoa Magugu Maji Ziwa Victoria Dkt. Kaniziro Manyika amesema magugumaji hayo yameathiri mifumo ya ikolojia, shughuli za usafiri na usafirishaji na shughuli za uvuvi katika ziwa Victoria na kubainisha kuwa Kwa kipindi cha Mwezi Februari hadi kufikia tarehe 18 Mei 2025 kiasi cha tani 840 kimeopolewa, zoezi hilo limesaidia kuondoa changamoto ya usafiri na usafirishaji katika eneo la Kigongo-Busisi.
Awali, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhandisi Cyprian Luhemeja amesema Katika kushughulikia changamoto hiyo kwa kipindi cha muda mfupi jumla ya tani 840 za gugumaji jipya aina ya Salvinia molesta limeopolewa na kufungua njia ya usafiri na shughuli za kiuchumi katika eneo la Kigongo-Busisi.
Mhandisi Luhemeja ameendelea kwa kusema kwa sasa eneo hilo halina changamoto tena ya Gugumaji ya aina hii mpya na juhudi zinaendelea katika eneo hilo la Kigongo-Busisi za kushughulikia Gugumaji la Asili aina ya Lutende. Jumla ya Ekari 65 zimeshughulikiwa katika kipindi cha wiki moja na lengo ni kumaliza Ekari zote kabla ya tarehe 10 ya Mwezi Juni-2025.
Mkutano huo Umehudhuriwa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,kamati ya ulinzi na Usalama,Mbunge wa jimbo la Sengerema, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Viongozi wa Chama ngazi ya Mkoa,Wilaya na kata, Makatibu Tawala,Wakuu wa Idara na Vitengo,Maafisa Tarafa,Taasisi na Mashirika Binafsi,Vikundi vya Ngoma na Wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.