Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi Bw. Abdi Makange kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi amewataka Maafisa na Watendaji wa Kata kusimamia na kuhakikisha Watoto wa shule za Sekondari na Msingi wanapata Chakula kwa asilimia 100 Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Wito huo ameutoa Leo Juni 19, 2024 wakati akifungua kikao cha Tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa shughuli za Lishe katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa kipindi cha kuishia robo ya tatu ya mwezi Machi 2024 ili kuongeza ufaulu na mahudhurio ya Wanafunzi Shuleni kwani lishe bora inamchango mkubwa katika kuyafanikisha hayo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Dkt. Clement Morabu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Misungwi ameeleza kwamba utekelezaji wa mkataba wa shughuli za lishe unaendelea vizuri katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi hususani katika utoaji wa Chakula shuleni ambapo zoezi hilo limefanikiwa kwa asilimia 95 ambapo kati ya Shule 178 na Shule ambazo zimekuwa na changamoto tayari wameweka mikakati kwa kushirikiana na Watendaji wa Kata ambao ndiyo wasimamizi wakuu wa shughuli hiyo ili kufikia asilimia 100 ifikapo robo ya nne.
Dkt. Morabu ameeleza kwamba mbali na kushughulikia suala la utoaji wa chakula Shuleni Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imefanikiwa kuwafikia watoto wenye changamoto ya utapiamlo na kuwapeleka katika vituo vya afya ambako wameendelea kupatiwa huduma stahiki za Afya na watoa huduma za afya kwa ngazi ya jamii ambao pia wamekuwa wakishirikiana nao kwa ukaribu kufanikisha zoezi la lishe bora kama ilivyoelekezwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Kanyelele Bw. Thomas Shunashu amesema kuwa katika kata hiyo wameweka kipaumbele suala la lishe kwenye ngazi zote kwa sababu lishe bora ndiyo msingi wa kuondoa udumavu na kupunguza magonjwa nyemelezi na hivyo wamefanikiwa kutoa chakula kwa wanafunzi katika Shule za Msingi 7 na Shule za Sekondari 2 baada ya kuwahamasisha wananchi kupitia vikao na hatua hiyo imesaidia wanafunzi kuendelea kupata muda mwingi wa kujifunza.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata ya Nhundulu Bw. Msobi Daniel ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta mpango wa lishe bora nchini ili kuleta tija kwa jamii hususani wanafunzi kwa kuhimarika zaidi kitaaluma na kiafya.
Bw. Msobi Daniel amesema kwamba Shughuli ya lishe bora katika Kata ya Nhundulu imetekelezwa kwa asilimia 100 baada ya kuwashirikisha Wananchi kupitia mikutano ya hadhara ambapo Wananchi wa kila Kijiji wamejitoa kuchangia Chakula kwa ajili ya wanafunzi na hatua hiyo imeendelea kuongeza uelewa wa lishe bora kwa Wananchi kutokana na hamasa wanayoipata kutoka kwa Viongozi wao wakiwemo Wenyeviti wa Vitongoji.
Mganga Mkuu Wilaya ya Misungwi Dkt. Clement Morabu (kushoto)akiwa pamoja na Lucia Basili wakati wa Kikao cha Lishe kilichofanyika katrika Ukumbi wa Halmashauri ya Misungwi.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.