Shilingi Bilioni 3.3 zaendelea kutekeleza ujenzi wa miradi ya uboreshaji mazingira ya sekta ya Elimu ya awali na msingi pamoja na Sekondari kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023 kupitia mradi wa Boost na Sequip nchini na kupunguza kero kwa Wananchi Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Akizungumza kwa nyakati tofauti katika ziara ya kukagua miradi hiyo ya Boost Mwakilishi wa Shirika la Benki ya Dunia Dkt. Safari Aquiline ameridhishwa na utekelezaji wa miradi ya Boost na Sequip ambapo miradi hiyo ililetwa kwa lengo la kutoa elimu bora kwa Wanafunzi kupitia ujenzi wa Madarasa yaliyojengwa, ujenzi wa vyoo pamoja na madawati uliotekelezwa kwa Shule za Msingi 2 za Mwabebea na Shilabela pamoja na shule mpya ya Sekondari ya Mwambola na amempongeza na kumshukuru Rais Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kutoa fedha nyingi katika miradi ya elimu kwa muda mfupi na amefurahi kushuhudia miradi hiyo imetekelezwa vizuri na kwa kuzingatia viwango na ubora pamoja na suala uhifadhi na utunzaji wa mazingira na kuwataka kuendelea kubuni na kutatua changamoto zingine zilizopo ikiwemo ukosefu wa maji na nishati ya umeme.
Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya awali na msingi OR - TAMISEMI Bi. Susan Nusu akizungumza na Viongozi na Watendaji wakati wa ziara ya ukaguzi na uhakiki miradi ya Boost Sequip Wilayani Misungwi hivi karibuni.
Naye Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya awali na msingi OR- TAMISEMI Bi. Susan Nusu amepongeza juhudi za makusudi kwa Viongozi na Watendaji wa Halmashauri ya Misungwi kwa kufanya kazi kwa ushirikiano, weledi na uaminifu na kuhakikisha miradi ya Boost na Sequip inatekelezwa kikamilifu na kukamilika kwa wakati na viwango na ubora kwa kuzingatia maelekezo na miongozo ya Serikali na hatimaye kufikia lengo la kupunguza ama kuondoa adha na kero ya Watoto kutohudhuria shule kutokana na miundombinu na mazingira mabovu ya shule za msingi na Sekondari nchini.
Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu Archt. Chagu Ng’homa kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza amesema Watendaji wamejitaidi na kwa uaminifu mkubwa katika kuhakikisha miradi hiyo ya Boost na Sequip inakamilika na inazidi kwenda vyema kwa kujengwa kwa kiwango cha hali ya juu na ubora na hatimaye kukidhi na kujibu changamoto za watoto kutokwenda shule kutokana na uhaba wa majengo ya madarasa pamoja na madawati na mazingira mazuri ya kufundishia na kujifunzia.
Akitoa taaarifa ya utekelezaji wa miradi ya Boost na Sequip Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bw. Addo Addo Missama ameeleza kuwa Halmashauri imefanikiwa kupata fedha shilingi Bilioni 1.9 kujenga shule za awali na msingi mpya 2 na kukarabati shule zingine 7, sambamba na fedha shilingi Bilioni 1.4 zilizotumika kutekeleza miradi ya Sequip ikiwemo ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Mwambola iliyogharimu shilingi Milioni 584.2 pamoja na ujenzi wa miundombinu katika Shule za Sekondari zingine 5 ambapo Viongozi na Watendaji wamehakikisha fedha hizo zimetekeleza shughuli za ujenzi kwa wakati na kwa kasi ambayo inaridhisha ili kurahisisha shughuli pamoja na kuongeza kiwango cha ufaulu kwa Wanafunzi na kupunguza adha na kero kwa watoto kutembea umbali mrefu na msongamano darasani.
Bw. Addo Missama amesema fedha zilizotolewa na Serikali kwa mwaka 2022/2023 kwa ajili ya kutekeleza mradi ni shilingi Bilioni 1,512,500,000/= ambazo zilitolewa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya sekta ya Elimu msingi ambapo zimeweza kunufaisha na kujenga na kukarabati miundombinu na majengo katika shule za msingi 9 ambazo ni Shilabela, Mwabebea, Mwagiligili, Chatta, Igwata, Busegeja, Iteja, Kagera, na Nyabuhele .
Amefafanua kwamba Serikali ilitoa fedha shilingi Milioni 540.3 kujenga shule mpya ya msingi ya Shilabela pamoja na shule ya msingi Ntende kwa sasa shule ya msingi mpya ya Mwabebea ambayo pia imejengwa na kukamilika kwa shilingi Milioni 540.3 na shule za msingi 7 zilizobaki zimefanyiwa ukarabati wa miundombinu ya majengo pamoja na nyongeza ya kujenga majengo ya madarasa na vyoo hivyo zoezi la ujenzi limefanyika vizuri na kwa ubora unaoridhisha kupitia kamati za ujenzi, manunuzi na mapokezi.
Baadhi ya Wakazi na Viongozi wa Kata ya Misungwi akiwemo Bw. Jackson Farasi pamoja na Clement Matenya wamesema kuwa hapo awali watoto walikua wakipata adha kubwa wakiwa darasani kwani iliwabidi kujazana hatimaye hali hiyo kwa sasa imetatuliwa ambapo wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kuleta maendeleo katika sekta zote ikiwemo elimu, Afya na Maji na kumwomba aendelee na moyo huo ili kuwaletea maendeleo ya dhati Wananchi na kuiomba Serikali kuwezesha upatikanaji wa nishati ya umeme, huduma ya maji pamoja na kujenga uzio katika Shule mpya ya Sekondari Mwambola ili kuwalinda watoto wa kike kuondokana na adha ya kufanyiwa ukatili na kusoma kwa utulivu.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.