Watu wenye Ulemavu watakiwa kuchangamkia fursa za Mikopo ya asilimia kumi inayotolewa katika Halmashauri nchini kwa mapato ya ndani Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Misungwi Mhe,Petro Sabato kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe, Paulo Matiko Chacha, amewataka Watu wenye Ulemavu kutumia fursa za Mikopo ya asilimia 10 asilimia ambapo asilimia 2 ni ya Watu wenye ulemavu ili kujikomboa na kujikwamua kiuchumi..
Hayo yamesemwa tarehe 02/05/2023 wakati wa kikao cha kuhuisha Kamati ya Watu wenye Ulemavu ya Wilaya kilichofanyika katika Ukumbi wa Jengo la Bima Hospitali ya Mitindo Misungwi ambapo amewataka Watu wenye ulemavu kukopa na kurejesha mikopo hiyo isiyokuwa na riba ili kuweza kujikwamua kwa kufanya shughuli za maendeleo na kujipatia kipato ambapo mikopo hiyo inatolewa ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bw.Benson Mihayo amesema kuwa Mikopo ya asilimia mbili ipo kwa ajili ya Watu wenye Ulemavu na inakopeshwa bila riba kuanzia vikundi na hata kwa mtu mmoja moja, na kutoa wito kwa Watu wenye Ulemavu kuchangamkia fursa hiyo kwa kukopa na kurejesha kwa wakati ili kuwapa nafasi wengine ya kukopa na wazitumie fedha hizo kwa manufaa yenye kuleta tija.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Watu wenye Ulemavu Wilaya ya Misungwi Bw.Leonidas Mtawala amesema kuwa changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiwakabili ni ufinyu wa bajeti na sasa suala lipata ufumbuzi na kuwafikia Watu wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya vijiji na kupata idadi yao na kujua changamoto gani wanazipitia na kuzifikisha sehemu husika ili kupata ufumbuzi.
Vilevile Bw.Mtawala ameongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa Watu wenye Ulemavu kupatiwa elimu ya kutosha juu ya madhara ya kuficha watoto wenye mahitaji maalumu majumbani kwa kufanya hivyo wanawakosesha watoto hao kupata haki yao ya msingi ya elimu bora,lakini pia amesisitiza kuwa miundo ya barabara kutoka majumbani kwenda mashuleni kwa watoto wenye ulemavu si rafiki na jamii kutokuwa karibu na Watu wenye ulemavu bado ni changamoto kubwa,Hivyo ameiomba jamii kuwa karibu pamoja na kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha wanawabaini watu wenye ulememavu katika kaya zao.
Mratibu wa Shirika la APDM Bw.Malimi Luhanya kwa kushirikina na Shirika la SENSE International amesema kuwa kuwepo kwa Mabaraza ya Watu wenye Ulemavu ambayo yanashughulikia kero na hoja za watu wenye ulemavu kuanzia ngazi za vijiji yamekuwa mhimili mkubwa wa kuibua changamoto zinazowakabili katika sehemu ngazi za vitongoji na vijiji na kuiomba Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kutoa vipaumbele katika bajeti kwenye mabaraza hayo ili yaweze kutekeleza majukumu yake barabara.
Bi.Jesca Boniventura Mwenyekiti wa SHEVIWATA Wilaya ya Misungwi ameeleza kuwa kuhuishwa kwa kamati hiyo italeta tija katika utendaji kazi kwa watu wenye ulemavu kwa kutoa maoni yao na changamoto zinazowakabili na njisi gani wanavyo weza kushirikishwa katika shughuli mbalimbali za kijamii zinazowazunguka na kutambulika kutoka ngazi ya chini hadi kitaifa,wakati huo huo kuiomba Serikali kuendelea kutoa elimu hasa maeneo ya vijijini kuhusina kunyanyapaliwa kwa Watu wenye Ulemavu ili kuondokana na dhana potofu iliyojengeka miongoni mwa watu na kuona watu wote wana haki sawa.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri wa Wilaya ya Misungwi Bw.Philemoni John amesema mikopo ya asilimia 10 inatolewa katika Halmashauri zote nchini bila riba na asilimia 2 ni kwa watu wenye ulemavu ambapo amewaomba kuchangamkia fursa ya mikopo kwa lengo la kuzalisha faida endelevu ili kuweza kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na kuwa mpango mkakati wa kujikwamua sehemu moja kwenda nyingine,na ni ruksa kwa kikundi au mtu mmoja mmoja kukopa kwa watu wenye ulemavu. Bw.John amesisitiza kuwa moja ya vigezo vya Mikopo ni pamoja na uaminifu kwa mwanakikundi katika kukopa.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati Ulinzi ya Watu wenye Ulemavu Wilayani Misungwi wakiwa katika picha ya Pamoja walipokutana katika kuzindua kamati hiyo hivi karibuni katika ukumbi wa jengo la bima Hospitali ya Mitindo Wilayani Misungwi.
Baadhi ya ya Viongozi wa Kamati ya Ulinzi ya Watu wenye Ulemavu Wilaya ya Misungwi,aliyesimama ni M/kiti wa kamati hiyo Bw.Leonidas Mtawala,kulia kwake ni Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi, Bw.Petro Sabato na wa kwanza kushoto ni M/ki kamati ya Huduma za Kijamii na Diwani wa Kata ya Mbarika Mhe,Joel Ndogani
Viongozi wa Kamati ya Ulinzi ya Watu wenye Ulemavu Wilaya ya Misungwi,aliyesimama ni Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bw.Benson Mihayo akiongoza mjadala huo mapema wiki hii katika Ukumbi wa Hospitali ya Mitindo wakati wa uzinduzi wa kamati hiyo.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.