Baraza la Madiwani lapongeza juhudi ya ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa robo ya tatu kuishia mwezi machi 2022 Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri. Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe, Kashinje Machibya alieleza kwamba Baraza la Madiwani limepongeza na kuridhika na juhudi na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo kuishia mwezi machi Menejimenti wameweza kukusanya shilingi 1,803,249,490.01 = sawa na asilimia 71.45 kwa bajeti ya mwaka 2021/2022.
Mhe, Machibya amesema kwamba wametenga fedha kiasi shilingi 400,000,000/= za mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika Kata ya Nhundulu Kijiji cha Mwawile na fedha hizo zinakusanywa kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ikiwa nia asilimia 40 ya kupeleka kwenye miradi ya maendeleo na kutoa rai kwa Wananchi watoe ushirikiano na kutoa ushuru kwa ajili ya kuongeza mapato ya ndani na kuhakikisha Halmashauri inapata mapato ya kutosha na kukamilisha miradi iliyopangwa.
Akizungumza katika Baraza la Madiwani Mhe, Machibya ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha kwa ajili utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ikiwemo vituo vya Afya pamoja na ujenzi wa madarasa.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Misungwi Bw. Benson Mihayo amesema kwamba Menejimenti itaendelea kukusanya mapato kwa bidii ili kufikia malengo waliojiwekea katika Halmashauri ili kuendelea kutatua changamoto za Wananchi kwa kuwaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Bw. Benson Mihayo amesema kwamba Halmashauri katika kipndi cha kuishia mwezi Machi 2022 imeweza kukusanya kiasi cha shilingi 1,803,249,490.01 kutoka katika vyanzo vya ndani vya mapato sawa na asilimia 71.45 na kusisitiza kwamba Menejimenti wamejiwekea mikakati ya kuendelea kukusanya mapato na kuundwa kwa timu mbili za ukusanyaji mapato ambazo zimeanza na Kata ya Usagara na Kata ya Misungwi na zoezi linaendelea vizuri kwa asilimia 84 na kutoa wito kwa Watendaji wa Kata pamoja na Waheshimiwa Madiwani wawe mabalozi katika ukusanyaji wa mapato na kuelimisha wananchi umuhimu wa mapato.
Alifafanua kuwa fedha zinazoletwa na Serikali ni lazima zisimamiwe vizuri pamoja na miradi iliyopo ili iweze kuwaletea maendeleo Wananchi pasipo kuwa na upotevu wa fedha,na kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi ya fedha ambazo Serikali inaendelea kuzitoa ni kwa ajili maslahi ya Taifa.
Wakati huo huo Katibu wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Misungwi Bw.Mohamed Ally Chorage alisisitiza Madiwani wahakikishe wanasimamia fedha zote za miradi kwenye maeneo yao ili ziweze kuleta maendeleo kwa wananchi aidha aliwataka Waheshimiwa Madiwani kuhakiksha wanatimiza majukumu yao na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa manufaa ya Wananchi kwa ujumla,
Pia alisisitiza kuwa ni vizuri jambo lolote la kimaendeleo linapoenda kufanyika kwenye eneo husika ni muhimu Diwani apewe taarifa ili kutoa ushirikiano na kusikiliza changamoto za wananchi katika eneo lake.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Misasi Mhe, Daniel Busalu ameishukuru Serikali ya awamu sita kwa kuendelea kuleta fedha za miradi hususan sekta ya Elimu pamoja na miradi ya sekta ya maji inayoiendelea kutekelezwa na tayari fedha zipo zaidi ya bilioni 50, kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa kutekeleza miradi ya Maji katika maeneo ya Kata ya Ukiriguru, Bulemeji, na Nyanghomango na Nyamayinza.
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi wakiendelea kusikiliza mjadala na hoja mbalimbali katika Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.