Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza yaagiza Kamati ya ujenzi kufanya marekebisho mapema katika ujenzi wa machinjio ya Fella na Nyamatala zinazojengwa katika Kata ya Fella na Igokelo Wilayani humo.
Agizo hilo limetolewa katika ziara ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango iliyofanyika hivi karibuni kwa lengo la kukagua na kuona utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ambapo ujenzi wa machinjio hizo zinazogharimu zaidi ya shilingi 30,000,000/= ni miongoni mwa miradi ilyotembelewa na Wajumbe wa kamati hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Antony Bahebe amesema kwamba ujenzi wa miradi hiyo haukuzingatia vigezo na kufuata ramani ya majengo ya machinjio sambasamba na usimamizi mbovu wa Wataalam na Kamati ya ujenzi ya vijiji husika, hivyo kusababisha baadhi ya maeneo kutokujengwa vizuri na mengine kuwekwa kinyume na ramani za machinjio zinavyoelekeza.
“ Kwa kuzingatia ramani za ujenzi wa machinjio za Wizara, naona kuna baadhi ya maeneo hayakuzingatiwa katika ujenzi huu, mfano uwekaji wa Tarazo pamoja na Hooks ambapo Mifugo atanaswa wakati wa kuchinjwa, lakini pia mabomba yamewekwa pembeni na nje ya mtaro wa kutiririsha damu baada ya mifugo kuchinjwa na kutundikwa juu,” alieleza kwa msisitizo zaidi Mwenyekiti wa Hamashauri.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Antony Bahebe Masele ( kulia) akiongoza Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango katika ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika ziara ya ukaguzi wa miradi kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2019/2020, ambapo wameweza kukagua zaidi ya miradi tisa katika vijiji vya Wilaya ya Misungwi,
Wajumbe wa Kamati ya Fedha walishangazwa na hali ya maendeleo katika ujenzi wa machinjio hayo ya Fella na Nyamatala na kuhoji namna Kamati ya ujenzi pamoja na Wataalam wa Halmashauri walivyoshiriki kusimamia ujenzi huo na kueleza kwamba ni muhimu miradi yote itekelezwe na kusimamiwa kikamilifu kwa kuzingatia ramani na maelekezo kutoka kwa Mhandisi wa ujenzi ili kuwa na majengo yenye ubora na kiwango kinachoridhisha na kuwaomba kujenga uzio katika machinjio ya Nyamatala..
Mhe, Antony Bahebe aliwataka Wataalam pamoja na Kamati ya ujenzi ya Vijiji hivyo vya Nyamatala na Fella kuhakikisha wanasimamia na kukamilisha marekebisho yote ambayo yamebainishwa na Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango ili kuweza kukabidhiwa miradi hiyo na mafundi ujenzi na kuanza kutumika na ameshauri viongozi wa Serikali ya Kijiji cha Fella kuwa na mpango mkakati wa kuweka na kuimarisha ulinzi katika eneo la machinjio hayo na kuitunza iweze kudumu.
Akitoa maelezo kwa Kamati ya Fedha,Uongozi na Mipango, Afisa Mipango Wilaya, Bi, Anna Urio alisema kwamba ujenzi huo wa Machinjio zote umefanyika kwa ushirikiano wa Waatalam wa Halmashauri pamoja na Kamati ya ujenzi ambapo Idara ya Mipango walikuwa wanafanya ukaguzi na kushauri Kamati ya ujenzi kufanya marekebisho katika maeneo yaaliyoonekana na mapungufu hususani katika machinjio ya Nyamatala wameweza kuzuia malipo ya Fundi ujenzi yenye shilingi 1,400,000/= na kueleza kuwa zitalipwa mara baada ya Fundi huyo kukamilisha marekebisho aliyoagizwa na Menejimenti.
Bi, Anna Urio ameongeza kwamba Menejimenti kwa ujumla imepokea changamoto zote na itahakikisha zinashughulikiwa na kutekelezwa kikamilifu na kwa wakati ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho katika maeneo yaliyobainishwa kwa kutumia Fedha zilizopo ambazo zililenga kujenga na kukamilisha machinjio hayo kutokana na mchoro na ramani iliyokuwepo na kuhakikisha ujenzi wa machinjio hayo ya Nyamatala na Fella yanakamilika vizuri na kuanza kutoa huduma kwa Wananchi kama ilivyokusudiwa.
Kamati ya Fedha katika ziara hiyo imeweza kutembelea na kukagua zaidi ya miradi mingine nane ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali kuu , Mapato ya ndani ya Halmashauri na Michango ya Wahisani na nguvu za Wananchi ambayo ni pamoja na Mradi wa Ujenzi wa Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Misungwi wenye shilingi 158,000,000/=, Ukamilishai wa darasa shule ya Msingi Chata kwa shilingi 12,500,000/=,Mradi wa Ujenzi wa Wodi ya Wazazi katika Kituo cha Afya Mbarika kwa shilingi 152,000,000/=, Ujenzi wa Mradi wa Kitalu Nyumba kwa shilingi 15,850,000/=, U Mradi wa Ukarabati wa Jengo la Soko la Madini kwa shilingi 27,500,000/=,
Miradi mingine ni pamoja na Ujenzi wa mradi wa Jengo la ofisi za Halmashauri wenye shilingi 1,000,000,000/=, Mradi wa Ujenzi wa Maabara ya Kemia na Biolojia Shule ya Sekondari Idetemya kwa shilingi 157,187,744/= na Ujenzi wa vyumba vitatu vya Madarasa katika Shule ya Sekondari J. Magufuli kwa nguvu za Wananchi na miradi yote imekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
Jengo la Maabara ya Kemia na Biolojia lilojengwa na Wahisani katika Shule ya Sekondari Idetemya,ujenzi huo wa Maabara hayo umegaharimu kiasi cha shilingi Milioni 157 hadi kukamilika
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.