Shirika la la kutetea haki za Wanawake na Watoto la Kivulini la Mkoani Mwanza lakabidhi Vifaa vya kusaidia mapambano ya kujikinga na kukabiliana na maambukizi ya Ugonjwa wa Corona utokanao na Virusi vya COVID 19 kwa Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Akizungumza katika hafla ya mapokezi ya vifaa hivyo , Mkuu wa Wilaya ya Misungwi ,Juma Sweda amewasihi na kuwakumbusha Wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Ugonjwa huu hatari wa Corona kwa kuvaa barakoa, kunawa mikono, kuepuka misongamano, na kuwataka kuzingatia maelekezo na kanuni zinazoendelea kutolewa na Wizara ya Afya kupitia kwa Wataalam wa Afya ili kuweza kujinga na maambukizi ya virusi hivyo.
Juma Sweda amewataka Wananchi kuendelea kuchapa kazi sambamba na kujikinga na Ugonjwa huu, amehimiza Wananchi kwenda mashambani kwa ajili ya mavuno ya mpunga na Kilimo cha Dengu kwa msimu wa mwaka huu, amepiga marufuku Wananchi kukaa viweni na kucheza bao na michezo ya Karata.
Akikabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI, Yassin Ally amesema Shirika limetoa vifaa hivyo kwa lengo na mkakati wa Kampeni ya kuwajengea ulewa Wananchi na kutokomeza Ugonjwa huo katika maeneo ya Mkoa wa Mwanza, vifaa hivyo ni pamoja na matanki na mapipa makubwa mawili ya kuwekea maji ya kunawa mikono , vifaa vya kupima joto la mwili vinne (4) na Printa moja ambavyo vyote vina thamani ya shilingi Milioni 3. 2.
Mkurugenzi Yassin amebainisha kwamba vifaa hivyo vinastahili kupelekwa na kutumika katika maeneo yenye mahitaji makubwa ikiwa ni pamoja na ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, maeneo ya Soko la Gwambina Misungwi, Mnada wa Misasi, pamoja na Kituo cha Polisi Wilaya kwenye Kitengo cha Dawati la jinsia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kisena Mabuba amewashukuru Wadau wa Shirika la KIVULINI kwa msaada walioutoa kwa Halmashauri ya Misungwi ambao ni dhahiri utasaidia sana Wananchi kunawa mikono kwa wingi katika maeneo ya masoko na minada ya Misasi na Misungwi, na kuwaomba Wadau wengine kuendelea kuunga juhudi za Serikali katika kukabiliana na janga hili kwa kutoa vifaa muhimu ikiwemo barakoa ambazo zitatumika kwa Waatalam wa Afya katika kujikinga wakati wa kutoa huduma kwa Wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda akinawa mikono katika tanki la kunawa mikono lilitolewa na Shirika la KIVULINI kwa ajili ya matumizi ya Wananchi hususan wateja wanaohitaji huduma za ukatili wa kijinsia katika Dawati la jinsia KItuo cha Polisi Wilaya ya Misungwi.
Mkurugenzi wa Shirika la KIVULINI Mkoani Mwanza, Yassin Ally akimkabidhi Printa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda iliyotolewa kwa ajili matumizi ya ofisi ya Kitengo cha Dawati la jinsia katika Kituo cha Polisi Wilaya ya Misungwi mapema jana, Printa hiyo itasaidia katika masuala ya kuweka na kutoa taarifa za Wananchi wanaofanyiwa vitendo vya ukatili katika jamii.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0718 530108
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.