Walengwa 1,976 wa Kaya maskini wametakiwa kujitokeza kuhakiki katika mfumo mpya wa matumizi ya Vishikwambi kwa ajili ya kukidhi na kupata vigezo vya kupokea malipo ya ruzuku ya fedha zinazotokana na mpango wa TASAF awamu ya tatu kipengele cha pili katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Hayo yamebainika na kuelezwa mapema leo katika mafunzo ya siku moja, yaliyofanyika katika Ukumbi wa MGS Hoteli –Misungwi kwa ajili ya kuwawezesha Wawezeshaji 33 wa ngazi ya Wilaya ambao wanatakiwa kufanya uhakiki wa walengwa wote waliopo katika Kaya hizo maskini 1,976 kwa kuzingatia masharti na vigezo na sifa zilizowekwa kwa Kaya zinazotakiwa kupata fedha za ruzuku kulingana na hali na maisha yao.
Akizungumza na Wawezeshaji wakati wa mafunzo hayo, Afisa mafunzo wa Mpango wa kunusuru Kaya maskini TASAF Makao makuu, Bi. Catherine Kisanga alisema mafunzo hayo ni kwa ajili ya maandalizi ya kwenda kuanza zoezi la siku mbili la la uhakiki wa Kaya maskini 1,724 ambazo hazikuhakikiwa awali pamoja na Kaya 252 ambazo zilikuwa zimesimamishiwa malipo mwanzoni, kutokana na sababu hizo hivyo katika zoezi hili la uhakiki huu wa awamu ya pili ni matarajio ya kuhakiki Kaya maskini 1,976 katika vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi zilizobaki katika uhakiki wa kaya katika mpango wa TASAF awamu ya tatu kipengele cha pili..
Bi. Kisanga amewataka Wawezeshaji wa ngazi ya Wilaya kuhakiki kwa umakini Kaya maskini za Walengwa wa mpango wa TASAF Wilaya ya Misungwi ili kupata taarifa sahihi za walengwa, kuhakikisha wanatumia mbinu mbadala na za kisasa za kufanya kazi na Jamii ambayo ina Wananchi tofauti na wenye uelewa, fikra na mawazo tofauti tofauti na kuhakikisha wanapata taarifa za kweli na kuwa waaminifu na waadilifu katika ujazaji wa takwimu na taarifa za walengwa wa kila Kaya maskini.
Bi. Kisanga amewataka wawezeshaji hao kutumia kikamilifu na kwa uaminifu mkubwa Vishikwambi ambavyo vimeleta tija ya kufanya kazi kwa weledi na kutoa taarifa na takwimu za walengwa wa Kaya kwa usahihi
"Ili kupata takwimu sahihi amewataka wawezeshaji hao wa mpango huo kufanya kazi kwa weledi na kufuata sheria ikiwa kila mmoja amekula kiapo cha kufanya kazi kwa kufuata sheria na nitoe rai tu kwamba kila mlengwa apatiwe huduma bora na niwatake mtumie lugha nzuri kwa walengwa na hata wale waliotolewa kwenye mpango huu muwaeleweshwe na kuwaelekeza kwa lugha nzuri na yenye staha ". Bi. Kisanga ameeleza na kuwasihi Wawezeshaji hao.
Naye Afisa ufuatiliaji wa TASAF III Wilaya ya Misungwi Steven Samwel alisema kwamba katika uhakiki huu wa walengwa utafanyika katika vijiji 60 tu vilivyokuwa vinapata fedha za ruzuku ya awali na kwamba zoezi hili litakapokamilika na kama kuna mlengwa wa Kaya maskini ambaye hataweza kujitokeza basi atakuwa amejiondoa mwenyewe na kupoteza sifa na fursa katika mpango wa kupata fedha za kujikimu za mpango huu.
Bw. Steven Samwel amefafanua zaidi kwamba maboresho yaliyofanyika katika uhakiki wa kaya hizi ni pamoja na mabadiliko ya maeneo ya kiutawala ikiwa ni pamoja na kijiji kilichoanzishwa upya na kijiji kingine basi kila kimoja kitajitegemea pamoja na kuwapatia taarifa kila kaya ili kurahisisha kukamilika kwa wakati zoezi hili.
Afisa Ufuatiliaji wa Mpango wa kunusuru Kaya maskini TASAF Wilaya ya Misungwi, ameongeza kwamba katika uhakiki wa awali Kaya za Walengwa 6,843 zilihakikiwa na baadae Kaya maskini 6,764 zilipatiwa na kupokea mgawo wa fedha za malipo ya mwezi Julai hadi Oktoba mwaka huu 2020 kiasi cha shilingi 269,612,000/= kwa awamu mbili ambazo ni sawa na shilingi 539,224,000/=
Kwa upande wake Mratibu msaidizi wa Mpango wa kunusuru Kaya maskini TASAF III wa Wilaya ya Misungwi Bi. Abigaeli Gimbagu alipohojiwa na Timu ya Habari, alifafanua kwamba awali kulikuwa na changamoto kwa baadhi ya walengwa kutoonekana kwenye eneo la tukio na baada ya kufuatilia tulipata sababu kuwa ni wagonjwa, wengine wapo safarini, na changamoto mbalimbali za kifamilia hivyo zoezi halikukamilika kutokana na kutowafikia walengwa zaidi ya Kaya 8,567 zilizokuwepo awali hivyo sasa tunaenda kwenye uhakiki wa mwisho kumalizia idadi ya walengwa ambao walikosa huduma hiyo kipindi kilichopita ambao ni kaya maskini zipatazo 1,976..
Mwezeshaji wa ngazi ya Wilaya , Bw. Lucal Nonga alibainisha na kueleza vikwazo na changamoto.iliyosababisha kutofanikiwa kumaliza zoezi la uhakiki kipindi kilichopita ni pamoja na watu kutokujitokeza kuhakiki kwa wakati na pia kuwatuma watu wasio na Vitammbulisho halisi vya uraia na mpiga kura na kusababsha kutomalizika kwa walengwa ila kwa sasa tutamaliza kutokana na elimu tuliyopatiwa imetuongezea tija ya kwenda kufabya kazi kwa weledi zaidi.
"Kupitia vishikwambi sasa mtu mmoja anaweza kuhakiki idadi ya watu 200 kwa siku na moja kwa moja ataingia kwenye mfumo rasmi wa uhakiki kwa njia mpya ya Teknolojia na kupunguza muda wa kufanya kazi kwani vinasaidia kuboresha taarifa sahihi na kwa wakati husika". Alieleza kwa msisitizo Mwezeshaji Nonga.
Baadhi ya Wawezeshaji wa ngazi ya Wilaya wakiendelea kupata mafunzo ya Mpango wa TASAF kwa ajili ya uhakiki wa Kaya maskini Wilayani Misungwi
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.