Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Emmanuel Tutuba akiakagua mradi wa Ujenzi wa Jengo la ofisi za Halmashauri Wiaya ya Misu ngwi, akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Kisena Mabuba pamoja na Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi, Petro Sabattona baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo.
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza waagizwa kuwajibika na kutatua migogoro na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji wa shughuli za miradi ya maendeleo inayotekelezwa Wilayani Misungwi.
Wito huo umetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Tutuba wakati akizungumza jana katika kikao na baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jengo jipya la Halmashauri.
Alisema kwamba ni muhimu sana kwa Watumishi wa umma kuwajibika katika majukumu na kuushauri uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kuweka utamaduni na utaratibu wa kufanya vikao na kukutana mara kwa mara kwa Watumishi kujadili mada na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maeneo ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali, wadau na michango ya Wananchi.
Bw, Tutuba amewataka pia Watumishi kupitia Idara na sekta mbalimbali zikiwemo sekta ya Ardhi, maendeleo ya jamii, Kilimo, na manunuzi na Ugavi kuhamasisha na kusimamia sheria na taratibu na kuzingatia utawala bora pamoja na kutatua na kutoa ufumbuzi wa migogoro inayojitokeza katika utendaji kazi kwa ajili ya kuleta tija na maendeleo ya dhati kwa Wananchi.
Amewataka Watumishi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii katika kufanya mawasiliano baina yao pamoja na Wananchi ili kuepuka na kuondokana migogoro ya ndani na nje ya ofisi, badala yake wajitambue na kutumia madaraka na mamlaka yao vizuri kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni na kuwa mfano katika jamii kupitia tabia, utendaji kazi na mienendo ya kila siku.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi, Petro Sabatto alimpongeza Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza kwa maamuzi na mikakati ya kutembelea katika Halmashauri za Mkoa wa Mwanza na kufanya vikao na Watumishi wa umma kwa lengo la kutoa uzoefu, kutatua na kupata ufumbuzi wa masuala na miradi mbalimbali inayotekelezwa na kuwezesha Watumishi kubadilisha mawazo na fikra ili kuimarisha na kuboresha utendaji kazi.
Awali Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza pamoja Viongozi na baadhi ya Wakuu wa Idara walifanya ukaguzi na kutembelea miradi ya maendeleo ya sekta ya Afya na utawala ambayo ni mradi wa ujenzi wa majengo mawili ya maabara na jengo la Wagonjwa wan je (opd) unaondelea kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Misungwi ambapo ameridhishwa na hatua ya ujenzi huo na kuwataka kuongeza kasi zaidi ili ukamilike kwa wakati.
Wakati huo huo pia amekagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ambao kiujumla umefikia asilimia hamsini za utekelezaji na kuridhishwa na maendeleo ya Mkandarasi anayejenga mradi huo ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania sambamba na usimamazi wa wahandisi na wataalam wa Halmashauri.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.