Kata ya Mondo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza yaibuka Kidedea kwa kuongoza katika ushindi wa mafanikio kupitia Sekta ya Elimu na Kilimo cha Zao la Pamba kwa mwaka huu 2018.
Hayo yamebainishwa katika Ziara ya Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,Mhe,Juma Sweda wakati akizungumza na Wananchi wa Kata ya Mondo kwenye Mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Mwaniko, ambapo kwa mujibu wa taarifa ya mafanikio ya Kilimo cha Pamba iliyotolewa na Mkaguzi wa Pamba wa Wilaya ya Misungwi, Bw,Azalia Sanga alisema kwamba katika msimu wa mwaka 2017/2018 Wakulima waliweza kulima na kuzalisha tani 2013 za Pamba ambapo kwa msimu wa mwaka 2016/2017 wakulima walizalisha tani 1040.
Mkaguzi wa Bodi ya Pamba wa Wilaya ya Misungwi,Bw,Azalia Sanga kwa niaba ya Afisa Kilimo.Ushirika na Umwagiliaji, Bw, Majid Kabyemela aliwasilisha taarifa ya mchakato wa kumpata Mkulima Bora kwa msimu wa mwaka 2017/2018 na kueleza kuwa mchakato huo ulianza mara moja mwezi Februari 2018 kwa kutumia Vikosi kazi vya Vijiji, na Kata na kuhitimishwa na timu ya Wataalam kutoka ngazi ya Wilaya ambayo ilichuja majina ya Wakulima 12 na kubaini Wakulima watano waliofanya vizuri zaidi na kulima kwa tija kwa kila Ekari ambapo mshindi bora Bw, Swalala Charles Nteminyanda mkazi wa Maganzo Kata ya Mondo aliibuka kidedea kwa kupata asilimia 98 kwa kuvuna Kilogramu 725 kwa Ekari.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,Mhe,Juma Sweda amemkabidhi Zawadi ya Pikipiki na kumpongeza Mkulima huyo bora wa Pamba kutoka Kata ya Mondo kwa kulima kisasa na kwa tija na kumwomba aendelee na kuongeza bidii zaidi katika msimu huu wa 2018/2019, amewataka pia Wakulima wengine Wilayani Misungwi kuiga mfano huo wa kufufua na kuendeleza zao la Pamba ili kuweza kuinua na kukuza uchumi wa Wananchi Wilayani humu na taifa kwa ujumla.
Mkulima bora wa msimu wa 2018 Bw, Swalala Charles Nteminyanda akifurahi mara baada ya kukabidhiwa Zawadi ya Pikipiki na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi,Juma Sweda (Kulia)
Mhe,Juma Sweda awali katika Ziara ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo aliridhishwa na utekelezaji wa miradi katika Kata ya Mondo na Mwaniko na kuwapongeza Viongozi na Wananchi wa maeneo hayo kwa kujitoa kuchangia na kusimamia kikamilifu shughuli za miradi, ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kufuatilia na kutoa fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa Majengo ya madarasa katika Shule ya Msingi Nyasato ili Wanafunzi waweze kuhamia na kuanza kusoma Shuleni hapo mapema mwaka 2019 pamoja na kutenga bajeti ya fedha za mapato ya ndani kuwezesha ujenzi wa Majengo ya Kituo cha Afya cha Mondo kinachoendelea kujengwa kwa michango na nguvu za Wananchi.
Jengo la vyumba viwili vya Madarasa vilivyojengwa kwa nguvu za Wananchi hadi hatua ya boma katika Shule mpya ya Nyasato,ujenzi huu unahitaji fedha kwa ajili ya ukamilishaji
Mhe Sweda amewapongeza pia Viongozi wa Kata ya Mondo na Mwaniko na uongozi wa Shule ya Sekondari Mwaniko kwa kuongoza kiwilaya kwa kuwa wa Kwanza kati ya Shule za Sekondari 23 kwa kufaulu kuanzia daraja la Pili hadi daraja la Nne katika Mitihani ya Kidato cha Nne mwaka 2017/2018 na kupata nafasi ya 31 kimkoa, na kuwataka kuendeleza ufaulu huo na kuinua kiwango na kuimarisha Sekta ya Elimu Wilayani na nchi nzima.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.