Katibu Tawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani Wilaya ya Misungwi Bw. Abdi Makange ametoa rai kwa Wananchi na vyama vya siasa kuzingatia umuhimu wa kusoma kanuni za Uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji na Vitongoji katika Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Rufani ya Uchaguzi wa Serikali za mitaa kilichofanyika katika ofisi ya Katibu Tawala Wilaya Bw. Abdi Makange amesema kuwa Kamati hiyo ina jukumu la kutenda haki na kuhakikisha kwamba malalamiko yoyote yanayojitokeza yanashughulikiwa kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya uchaguzi, hii ni muhimu sana ili kujenga imani miongoni mwa Wananchi kuhusu mchakato wa Uchaguzi na matokeo yake ambapo elimu kuhusu kanuni za Uchaguzi inapaswa kutolewa kwa Wananchi ili waweze kuelewa haki zao na wajibu wao katika uchaguzi utakaofanyika mwaka huu Novemba 27, 2024.
"ni wajibu wao kuelimisha wanachama wao kuhusu kanuni za uchaguzi na kuhimiza ushirikiano na Kamati za Uchaguzi katika ngazi zote, hii itasaidia kupunguza migogoro na malalamiko ambayo mara nyingi yanajitokeza wakati wa Uchaguzi, alihimiza kuongeza ushirikiano na Wananchi na vyama vya siasa, Kamati hiyo itahakikisha kuwa Uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu" Amesema Bw. Abdi Makange
Bw. Makange amewataka Wananchi wote kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi, wakijua kuwa sauti zao zina thamani na zinachangia katika maendeleo ya jamii zao alisisitiza kuwa, ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha kuwa Uchaguzi unafanyika kwa haki na uwazi, ili kuleta maendeleo endelevu katika Wilaya ya Misungwi.
Naye Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa ngazi ya Wilaya, kwa niaba ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Halmashauri ya Misungwi Bw. Stephen Singira, ameeleza umuhimu wa Kamati ya Rufani katika mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za mitaa ambapo Kamati hiyo inatarajia kupokea mapingamizi yote yanayohusiana na Wagombea wa nafasi mbalimbali, na kwamba itazingatia miongozo iliyowekwa ili kutoa suluhu sahihi, ameongeza kuwa lengo la Kamati hiyo ni kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa uwazi na haki, ili kuimarisha amani miongoni mwa jamii na Wananchi katika uchaguzi.
Bw. Singira alitoa wito kwa vyama vya siasa kuzingatia na kusoma kwa makini kanuni za uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za Mitaa, hususan ngazi ya vijiji na vitongoji, ameeleza kuwa uelewa mzuri wa kanuni hizo utasaidia kupunguza migogoro na malalamiko wakati wa uchaguzi, na hivyo kuimarisha demokrasia katika ngazi za chini za utawala. Kamati ya Rufani inatarajia kufanya kazi kwa karibu na wadau wote ili kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na utulivu.
Naye Afisa uchaguzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Bw. Dickson Kawovela, ameeleza kuwa mgombea anaweza kupata haki zake kupitia Sheria za Serikali za mitaa, hususan kifungu cha 15 na 16 cha sheria ya Serikali za mitaa (mamlaka za wilaya) sura ya 287 na 288. Kifungu cha 15 kinataja sifa zinazotakiwa kwa mgombea, ikiwa ni pamoja na kuwa na uraia wa Tanzania, umri wa kutosha, na kuwa na elimu inayotakiwa ambapo kifungu cha 16 kinabainisha sababu ambazo zinaweza kumfanya mgombea kupoteza sifa yake, kama vile kutokuwa na sifa zilizotajwa katika kifungu cha 15 cha sheria hiyo..
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Rufani wamesema kuwa ni umuhimu wa kufuata sheria hizi ili kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa wa haki na uwazi ambapo ni jukumu la kila mgombea kujihakikishia kuwa anatimiza sifa zote zilizotajwa ili kuepuka matatizo yanayoweza kujitokeza wakati wa mchakato wa uchaguzi ambapo wagombea wanapaswa kuzingatia sheria hizi ili kulinda haki zao na kuhakikisha kuwa wanashiriki katika uchaguzi kwa njia sahihi.
Kauli mbiu ya Uchaguzi wa Serikali za mitaa Mwaka huu 2024 inasema kuwa “Serikali za Mitaa Sauti ya Wananchi, Jitokeze kushiriki Uchaguzi Novemba 27, 2024”.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.