Kamati ya Lishe ya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi yawataka Watendaji wa Kata na Vijiji kufanya maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe ya Kijiji kwa ajili ya kutoa Elimu ya Shughuli za Lishe kwa Wananchi katika Halmashauri ya Misungwi Mkoani Mwanza.
Akizungumza mapema katika kikao hicho leo tarehe 28 Februari 2025 Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe Bw. Clement Morabu ambaye ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Misungwi amewataka Wajumbe na Wakuu wa Idara kuendelea na ufuatiliaji na usimamizi wa hali ya Lishe katika maeneo yao na kukamilisha uwekaji wa Bajeti ya shughuli za Lishe katika Mpango na Bajeti ya mwaka ujao 2025/2026, kuzisisitiza Idara ya Elimu msingi na Sekondari kuhakikisha wametenga fedha za kutosha kutekeleza shughuli za Lishe mashuleni ili kuwapatie Lishe bora Watoto na Wananchi wa Misungwi na kuwahimiza Watendaji wa Kata na Vijiji kutekeleza maelekezo na maagizo yanayotolewa hususani suala la maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe ili Wananchi waendelee kupatiwa Elimu na kufahamu faida za Lishe.
Kwa upande wake Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bi. Lucia Bazili wakati akiwasilisha taarifa ya viashiria vya utekelezaji wa Maendeleo ya shughuli za Lishe Wilayani Misungwi na kadi alama, ameeleza kwamba hali ya utoaji wa Lishe katika shule za msingi na Sekondari imeendelea kuimarika kwa kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2024/2025 inayoishia Disemba 2025 na watoto wanaendelea kupata mlo mmoja wakati wa masomo na Wazazi na Wananchi wamehamasika katika suala la uchangiaji wa Chakula mashuleni.
Amewataka na kuwakumbusha Watendaji wa Kata na Vijiji wa Halmashauri kufuatilia na kusimamia utekelezaji pamoja na kuhakikisha wanafanya Maadhimisho ya siku ya Afya na Lishe ambayo kwa mujibu wa taratibu na sharia hufanyika mara moja kwa kila robo ya mwaka kwa lengo la kutoa Elimu na hamasa ya shughuli za Lishe kwa Wananchi ili kuweza kufikia malengo ya Mkataba wa Lishe.
Katika kikao hicho cha Kamati ya Lishe ngazi ya Halmashauri kimewashirikisha Wakuu wa Idara na Wataalam mbalimbali kutoka sekta za afya, elimu, kilimo, na maendeleo ya jamii, Fedha, Mipango na Ufuatiliaji, Habari na Mawasiliano pamoja na Utawalana raslimali watu.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.