Wajumbe wa Kamati ya Fedha,Uongozi na Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza wamekagua na kupongeza utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotekelezwa kwa fedha za Serikali, Wafadhili pamoja na Michango na nguvu za Wananchi Vijijini.
Kamati ya Fedha,Uongozi na Mipango imefanya ziara hiyo kwa ajili ya kukagua miradi na shughuli mbalimbali zilizotekelezwa kwa kiapindi cha robo ya pili kuanzia mwezi Oktoba hadi Disemba mwaka 2018 na zinazoendelea kutekelezwa na kuona hali halisi ya utekelezaji na kutatua changamoto zilizopo pamoja na kushauri namna ya kukamilisha miradi husika kwa viwango, ubora na kwa wakati .
Akizungumza katika ziara hiyo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe,Paulo Kishinda alipongeza kazi inayofanywa na Menejimenti katika utekelezaji na usimamizi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa vijijini akitoa mfano katika mradi wa ujenzi na ukarabati wa maabara katika Sekondari ya Paulo Bomani ambao ujenzi upo katika hatua za ukamilishaji, na kazi zilizofanyika ni pamoja na ukarabati wa majengo matatu, upigaji lipu, marekebisho ya mfumo wa Gas, kuweka mfumo wa maji safi na taka na mfumo wa umeme na kazi imefanyika kwa kutumia mafundi wenyeji kwa gaharama ya shilling Millioni 50.
Mhe,Kishinda amesema kwamba baadhi ya miradi inaonekana kuwa na changamoto za utekelezaji na kusababisha kuchelewa kukamilika ukiwemo mradi wa ujenzi wa choo katika Shule ya Msingi Kigongo kwa gaharama ya shilingi Milioni 30, ambao umeanza tangu mwaka 2018, amewataka uongozi wa Shule na Menejimenti kufanya haraka ili mradi huo ukamilike ndani ya mwezi Machi 2019 na Wanafunzi waanze kutumia na kunufaika na mradi huo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri,Bi Anna Urioh ambaye pia ni Afisa Mipango wa Halmashauri alieleza kwamba Menejimenti imeendelea kutoa ushauri katika Kamati za ujenzi wa miradi mbalimbali hususani katika taratibu za ujenzi,manunuzi na kuelekeza taratibu na sheria zote zifuatwe ili kuweza kuwa na majengo bora na imara na Viongozi wa Kata na Vijiji wameelekezwa kufanya ufuatiliaji na usimamizi wa mara kwa mara na kutoa taarifa endapo mambo ya ujenzi na manunuzi hayaendi kikamilifu, pia timu ya wataalamu wa Idara ya ujenzi wameendelea kutembelea na kusimamia miradi husika na kutatua changamoto zinapojitokeza kwa wakati.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.