Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe. Johari Samizi, awataka Maafisa Ugani na wadau wa kilimo kuhamasisha matumizi ya mbegu bora ya zao la Pamba ili kuboresha uzalishaji wa zao la pamba nchini Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza
Akizungumza katika mafunzo yaliyofanyika tarehe 23 Septemba, 2024 katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Ukiriguru yanayofadhiliwa na Mradi wa Cotton Victoria ameeleza kwamba Mafunzo hayo yatawasaidia Maafisa ugani kutoa elimu kwa Wakulima kwa kina kuhusu mbinu bora za kilimo cha pamba, ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya mbegu bora, mbolea, na udhibiti wa magonjwa na wadudu hivyo ni muhimu kutumia teknolojia na utafiti wa kisasa ili kuongeza uzalishaji na ubora wa pamba, ambayo ni zao muhimu kwa uchumi wa eneo la Misungwi na Mkoa wa Mwanza kwa ujumla.
Mhe. Samizi amewataka Maafisa Ugani, pamoja na Wadau wa kilimo wanaopata fursa ya kujifunza na kushiriki maonyesho ya vitendo vya kilimo wapate namna ya jinsi ya kutekeleza mbinu hizo katika mashamba yao na Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kati ya Wakulima, taasisi za kilimo, na Wadau mbalimbali ili kuhakikisha Wakulima wanapata maarifa na rasilimali zinazohitajika kwa ajili ya kilimo chenye tija ili kuhakikisha mafanikio ya mradi wa Cotton Victoria project yanawanufaisha Wananchi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Ukiruguru, Dkt. Paul Saidia akitoa ufafanuzi kuhusu mafunzo ya Mbegu bora za zao la pamba yenye lengo la kuboresha uzalishaji wa pamba na kuongeza kipato cha wakulima tangu mwaka 2017na kubainisha kuwa Mafunzo haya yanahusisha Maafisa Ugani na wadau wa kilimo cha pamba kutoka maeneo mbalimbali, ambapo watajifunza mbinu bora za kilimo, usimamizi wa mazao, na matumizi sahihi ya mbegu bora zinazotolewa na mradi huo unaotarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya kilimo na kusaidia katika maendeleo ya jamii na kusaidia wakulima kuongeza mavuno yao na kuboresha ubora wa pamba wanayozalisha na umuhimu wa kutumia mbegu bora ambazo zimepatiwa utafiti wa kisayansi ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na magonjwa yanayoathiri zao hili.
Naye Mratibu wa Mradi wa Cotton Victoria kutoka Chuo Kikuu cha Lavras (UFLA), Prof. Pedro amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Misungwi kwa kushiriki katika mafunzo ya namna bora ya kutumia mbegu za pamba, na kusisitiza umuhimu wa elimu kwa Wakulima katika kilimo cha pamba, na kwamba yatawasaidia Wakulima kuongeza uzalishaji na kuboresha ubora wa mazao yao na kuomba ushirikiano kati ya Serikali na taasis katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya kilimo katika maeneo hayo
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.