Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi amewaagiza Watendaji na Maafisa Afya kusimamia kikamilifu usafi wa mazingira kwa ubunifu na kutoa elimu pamoja na kuhamasisha Wananchi kujenga vyoo bora Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Mhe. Johari Samizi ametoa agizo hilo tarehe 15/07/2024 wakati wa kikao cha Tathmini ya hali ya usafi wa mazingira katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ambapo amewataka Watendaji wa Kata na Maafisa Afya kuhamasisha na kutoa elimu kwa Wananchi kwenye Kaya zao kujenga vyoo na kuvitumia kikamilifu na kufanya kazi kwa ubunifu kwa kuwashauri Wananchi kupitia kwenye Kaya mbili au tatu washirikiane kutoa fedha za Saruji kwa ajili ya kujenga au kuboresha boma la choo bora kwa kutumia ramani halisi ya choo bora kulingana na vipimo na kuwasihi waendelee kutoa elimu kwa Wananchi kushirikiana kujenga vyoo pamoja na kuendelea kuhubiri suala la usafi wa mazingira katika familia na maeneo ya umma.
“ Kwa nini tuzalishe taka halafu hatujui tunazipeleka wapi, taka zinazalishwa lakini hamna dampo kuna faida gani, hivyo Wataaalam wajifunze kupitia maeneo mengine kama Njombe na Makete ambapo watu ni wasafi mpaka ngazi ya familia ni kwamba Wataalam waliamua kulibeba jambo likawa ni la kwao, wakaliimba, wakalihubiri , na Wananchi wakalipokea kwa mapenzi na mikono miwili wakalitekeleza,s sijui inaeleweka vizuri , ebu tufanye, Wananchi hawa ni wasikivu na waelevu kwa sababu kazi ya usafi ni ya kila siku si jambo la kukumbushana, lakini ukifuatilia sana kwenye maeneo yetu maeneo ya umma ndo machafu zaidi kuliko hata maeneo ya watu wanapoishi”. Alizungumza kwa msisitizo Mhe. Johari Samizi.
Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe, Johari Samizi amehimiza Wataalam na Watendaji kusimamia vikundi vya wafanya usafi wasimaamie kwa bidii ili usafi ufanyike ipasavyo na kufanya mazingira yote yawe safi na salama.
Naye Afisa Afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bi. Ivona Mabala ambaye ni Mratibu wa mradi wa Wash anayeshughulika na masuala ya Usafi na Mazingira katika Halmashauri ya Misungwi amewasisitiza Watendaji na Maafisa Afya kuendelea kupambana kuhamasisha Kaya zote kujenga vyoo na kuvitumia na kupitia mradi huu ambao unasaidia kuwezesha zoezi na mpaka sasa wameshafikia Vituo 40 kati ya 60 na tayari kupitia fedha walizovuna imewasaidia kuagiza gari ya shilingi Milioni 127 kwa ajili ya usimamizi wa mradi huu wa Wash ili kuendelea kuboresha usafi wa mazingira kwa Wananachi.
Bi. Ivona Mabala ameeleza kuwa Wananchi wote wa Wilaya ya Misungwi wanatakiwa kujenga na kuboresha vyoo na kuwa na vyoo bora na vya kisasa kupitia kila Kaya pamoja na kutunza mazingira yao kwa kufanya usafi wa mara kwa mara kwenye familia zao na maeneo ya biashara, taasisi za umma pia kwenye ofisi za Kata, Vijiji, na kuwaomba Watendaji na Maafisa Afya kwa kila mmoja kuhamasisha Wananchi kuhusu utunzaji wa mazingira katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila Kaya inakuwa na choo bora na kuvitumia kwa usahihi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bw. Christopher Legonda amewataka Watendaji wa Kata na Maafisa Afya kubadilika na kufanya kazi na kuacha tabia ya kufanya kazi kwa mazoea,kila mmoja afanye kazi kwa kipande chake alichopangiwa na kutokuwa wababaishaji na kuhakikisha kwamba usafi wa mazingira unafanyika kila siku na sio mara moja ya mwisho wa mwezi kama ilivyokua awali.
Bw. Legonda amesisitiza Watendaji hao kutimiza majukumu yao ipasavyo na kuwaonya baadhi ya Watendaji na Wataalam ambao hawakai katika Vituo vya kazi muda wote vitendo ambavyo vinapunguza uwajibikaji kwa mtumishi na kusababisha kuzorotesha juhudi za kuwapatia Wananchi maendeleo na kutotimiza malengo yaliyowekwa na Serikali kupitia sekta mbalimbali.
Picha za Viongozi na Watendaji wakati wakijadili kuhusu hali ya Utekelezaji wa mradi wa Wash katika usimamizi wa masuala ya ujenzi wa vyoo na Usafi wa mazingira
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.