Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Mhe. Johari Samizi, amewataka Watendaji kutekeleza na kusimamia miradi kikamilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni, na taratibu na kukamilisha miradi kwa wakati Wilayani Misungwi.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi ameyabainisha hayo Novemba 13, 2024 katika ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo ya sekta ya Elimu pamoja na Sekta ya Maendeleo ya jamii na Ufundi ambapo katika shule ya Sekondari Misungwi amekagua maendeleo ya ujenzi wa mabweni 2 ya Wasichana yenye thamani ya shilingi 281 pamoja na ujenzi wa shule ya Amali katika Kata ya Mabuki Kijiji cha Mhungwe itakayogharimu shilingi Bilioni 1.6 hadi kukamilika na maendeleo ya miradi hii iliyopo katika hatua za awali za msingi.
Mhe. Samizi ametembelea katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii na Ufundi (CDTTI) Misungwi na kupata taarifa za maendeleo ya ujenzi wa Jengo la ghorofa 4 la Hosteli ambalo linajengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 2.7 na tayari limejengwa hatua ya awamu ya kwanza ya msingi kwa fedha shilingi Milioni 300 na kuishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa miradi mbalimbali katika Wilaya ya Misungwi, Watendaji kuendelea kusimamia kikamilifu na kuongeza juhudi za ufuatiliaji wa miradi ili kuhakikisha Wananchi wanapata huduma bora na kwamba miradi inatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa na kuwahamasisha Wananchi kuanzisha miradi ya kimaendeleo, kama vile kilimo, ufugaji na biashara ndogo ndogo, ambazo zinaweza kuwasaidia kujipatia kipato kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kupitia Halmashauri.
“ ni muhimu kwa Watendaji wote kufuata na kuzingatia sheria, na miongozo iliyopo ili kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza ambapo kila mradi unapaswa kuwa na malengo yanayoweza kupimika, na kwamba ni wajibu wa kila Mtumishi kuhakikisha kuwa miradi inatekelezwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati”. Alisisitiza Mhe. Johari Samizi.
Mhe. Samizi pia alitoa wito kwa Wananchi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za mitaa ili kuhakikisha kuwa wanatambua haki zao za msingi na kuchagua kiongozi wanayemtaka ili kuchochea maendeleo na Uchaguzi wa Serikali za mitaa utafanyika Novemba 27, 2024, hivyo Wananchi wote waliojiandikisha kujitokeza kupiga kura na kuwachagua Viongozi wanaowataka kwa ajili ya kuleta maendeleo.
Naye Kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi Bi. Elly Makala amewasihi Viongozi na Watendaji kufanya kazi wa uadilifu na kuhakikisha wanazingatia taratibu, kanuni na sheria za shughuli za ujenzi kwa kufuata sheria za manunuzi na kufuatilia ujenzi wa miradi hiyo hatua kwa hatua hadi kukamilika ili kujenga kwa ubora na Viwango.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.