Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi awataka Watumishi na Wananchi kudumisha na kuendelea kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ameyasema hayo leo 26.04.2024 wakati akiongea kwenye mdahalo na Wanafunzi wa sekondari na wanachuo pamoja na watumishi katika ukumbi wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Misungwi wakati wa kuhitimisha kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha na kuenzi Muungano wa Tanzania.
Mhe.Johari Samizi amefafanua kueleza kwamba tunapoadhimisha miaka 60 ya Muungano wetu, Watanzania wote tuna kila sababu ya kutafakari na kutathmini masuala muhimu yaliyokusudiwa na Waasisi wa Taifa letu ambao walitia saini Hati ya makubaliano ya Muungano kwa niaba ya wananchi wa nchi hizo mbili. Pamoja na Waasisi wetu kutangulia mbele ya haki, misingi waliyotuachia imeendelea kuimarisha umoja, amani, na utulivu wa Taifa letu.
Aidha Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Misungwi ameongeza kuwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umejengeka kutokana na historia ya uhusiano wa udugu wa damu, harakati za pamoja na ushirikiano wa vyama vya ukombozi vya Tanganyika na Zanzibar katika kupigania uhuru.
Mhe.Samizi amesisitiza kuwa uchumi umeimarika kutokana na mazingira na mahusiano mazuri ya kibiashara kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.
“Tumeshuhudia kuimarika kwa miundombinu, hususan ya barabara na huduma za jamii ikiwamo afya, maji na elimu”.Alisema Mkuu wa Wilaya.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Wilaya amewataka wananchi kuthamini juhudi za Waasisi wa Muungano wetu na mafanikio yaliyopatikana kutokana na Muungano, kwa pamoja kuendelea kuuenzi, kuulinda na kuudumisha Muungano wetu Adimu na Adhimu.
Wanafunzi wa chuo cha Maendeleo ya jamii Misungwi wakifuatilia kwa ukaribu mdahalo wa sherehe za kilele cha Maadhimisho ya Muungano wa miaka 60 ya Tanganyika na Zanzibar Aprili,26,2024 katika ukumbi wa chuo hicho,ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe,Johari Samizi.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.