Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi awataka Wajasiliamali wa Vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu kutumia kwa tija mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali ili kujiimarisha na kukuza uchumi binafsi na jamii kwa ujumla pamoja na kuleta maendeleo kwa Wananchi Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi wakati akifungua Semina ya mafunzo kwa vikundi 41 vilivyokidhi vigezo vya kupatiwa mikopo ya asilimia 10 kutoka fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, amevitaka vikundi hivyo kukopa na kurejesha mikopo hiyo isiyokuwa na riba kwa wakati ambayo itawawezesha kujikwamua kiuchumi kwa kufanya shughuli za maendeleo na kujipatia kipato ambapo mikopo hiyo inatolewa kwa vikundi vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi.
Mhe. Samizi ametoa rai kwa vikundi hivyo kuwa wanapaswa kuzingatia utaratibu wa marejesho ya mikopo hiyo kwa kipindi na muda uliokubaliwa wa utekelezaji wa shughuli za vikundi hivyo na kuwataka Wataalam na Watendaji wa Serikali kutembelea na kukagua shughuli na miradi husika na kujionea namna ambavyo wanafanya kazi zao na wanavyonufaika na mikopo hiyo na kushauri namna bora ya kuendeleza miradi na biashara zao.
“Vikundi hivi vyote kuna orodha yake na mahali vilipo, jiandaeni nitapita kikundi kimoja baada ya kingine, kama mnatarajia mkishapewa fedha mtawanyike nitakapofika baada ya kutoa taarifa kikundi hicho hakipo, tafsiri yake hamna sifa kwa sababu mlisema uongo hakuna kikundi , hivyo mjiandae kurejesha fedha hizo na sheria itafuata mkondo wake”. Amewatahadharisha na kuwasisitiza Mhe, Johari Samizi .
Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Bw, Clement Morabu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Wilaya ya Misungwi Bw. Addo Missama wakati akiwasilisha taarifa fupi ya mafunzo ya mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu amesema kuwa katika kipindi cha robo ya pili 2024/2025 , Halmashauri Wilaya ya Misungwi kupitia dawati la uwezeshaji Wananchi kiuchumi imetoa mikopo wa shilingi Milioni 398,796,784/= ambayo ni sehemu ya mikopo ambayo imetolewa kwa vikundi 41 ambapo 13 ni vya Vijana, 24 vya Wanawake na Vikundi 4 vya watu wenye ulemavu ili kutekeleza shughuli za uzalishaji mali na kukuza uchumi kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini uliokithiri.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri Wilaya ya Misungwi Bi. Ester Msoka amesema kuwa ni vyema kutumia fursa za Mikopo ya asilimia 10 ili kujikomboa kiuchumi na mikopo hiyo inatolewa bila riba kupitia kikundi na hata kwa mtu mmoja moja, na kutoa wito kwa vikundi kuchangamkia fursa hiyo kwa kukopa na kurejesha kwa wakati ili kuwapa nafasi wengine ya kukopa na kuzitumiea fedha hizo kwa manufaa yaliyotarajiwa na yenye kuleta tija.
Wakati huo huo, Afisa Biashara wa Halmashauri Wilaya ya Misungwi Bi. Emmaculatha Kusekwa amewasihi vikundi hivyo kuhakikisha wanakuwa na leseni za biashara kabla ya kuanza shughuli zao na kuzingatia utunzaji wa kumbukumbu za mauzo na manunuzi yatayofanyika ili kuweka taarifa sahihi na kunufaika na fedha hizo za mikopo ya riba ya asilimia 10 kutoka Halmashauri
Katika hatua nyingine Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Wilaya ya Misungwi Bw. Charles Munthal amevitaka vikundi hivyo kuhakikisha wanakua na bima ikiwa wanahusika na ujasiliamali kupitia vyombo vya moto kama vile pikipiki ili kulinda usalama wao na wa abiria ambapo pia wanapaswa kutoa taarifa kwa jeshi la polisi ikiwa kuna aina yoyote ya kukosekana kwa usalama katika maendeo yao kwani jukumu la jeshi la polisi ni kulinda raia na mali zao.
Baadhi ya wanavikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu kwa nyakati tofauti tofauti wameishukuru Serikali na kutoa pongezi kwa kupatiwa Semina na kuahidi kuchangamkia fursa ya mikopo kwa lengo la kuzalisha faida endelevu ili kuweza kurejesha mikopo hiyo kwa wakati na kuwa na mpango mkakati wa kujipatia maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kuweza kutoka sehemu moja kwenda nyingine, na mpango mpya wa kuruhu kikundi au mtu mmoja mmoja kukopa kupitia kikundi kwa kuzingatia maelekezo yaliyotolewa na Serikali na kuahidi watafuata masharti na kanuni na kuhakikisha wanasimamia shughulina biashara zao na kurejesha fedha za mikopo kwa wakati..
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.