Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe, Veronika Kessy aagiza Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kuanza kukusanya Ushuru wa mapato yatokanayo na Masoko yote kuanzia Februari mosi mwaka huu ili kuongeza mapato ya ndani.
Akizungumza juzi katika kikao cha tathmini na kupokea taarifa ya uchambuzi wa mfumo wa usimamizi na uendeshaji wa masoko Wilayani Misungwi iliyotolewa na Ofisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Misungwi tarehe 09/01/2023 kwa lengo la kuboresha na kuongeza mapato ya Halmashauri ameeleza kwamba ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halamshauri kupitia Kitengo cha fedha na mapato wanatakiwa kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji wa ushuru katika masoko yote ikiwemo soko la Misungwi. Usagara, Nyashishi, na Bujigwa.
Taarifa ya uchambuzi ya masoko ilibainisha kwamba Menejimenti ya Halmashauri ya Misungwi kwa muda mrefu sasa imeshindwa kukusanya kikamilifu ushuru katika masoko hayo na badala yake Viongozi wa Serikali za vijiji pamoja na Wananchi wasiokuwa waadilifu wamekuwa wakitoza ushuru huo na mapato husika yamekuwa yakitumika kinyume na taratibu ambapo Halmashauri ndio yenye mamlaka na jukumu katika usimamizi na ukusanyaji ushuru kwenye masoko kwa mujibu wa sheria za fedha.
Mhe Veronika Kessy amekerwa na vitendo vya baadhi ya Viongozi, Wananchi na Watendaji wasiokuwa waadilifu waaminifu ambao wamekuwa wakikaidi katika kutekeleza shughuli za maendeleo ya Wananchi ambao wengine wamekuwa wakijihusisha na shughuli za Ukusanyaji wa ushuru wa usafi katika masoko kinyume na sheria na taratibu na kutowasilisha mapato hayo katika mfuko wa Halamsahuri.
Ameelekeza Jeshi la Polisi Wilaya ya Misungwi kuwahoji Mwenyekiti na Mtendaji wa Kijiji cha Misungwi na kutoa maelezo ya kina kuhusu ukaidi unaofanywa na Mwenyekiti huyo wa kijiji kwa kutotekeleza maagizo na maelekezo ya mara kwa mara kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhusu kuhusika kwake kuweka kikundi chake kinachohusika na usimamizi wa uzoaji taka na ukusanyaji wa ushuru wa Usafi majumbani na Soko la Misungwi Mjini na kuzuia kikundi halali kilichowekwa kisheria kukusanya na kufanya usafi wa soko hilo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halamshauri ya Wilaya ya Misungwi Bw, Benson Mihayo amesema kuwa Menejimenti kwa ujumla imepokea mapungufu yaliyobainishwa katika taarifa hiyo ya masoko na kwamba tayari ameshaanza kuchukua hatua na kuweka mikakati ya kukusanya kikamilifu ushuru huo kwa mujibu wa sheria katika masoko ya Usagara, Misungwi, Nyashishi na masoko mengine na kuondoa mianya yote ya upotevu wa mapato na kuhakikisha kuwa mapendekezo yote 19 yaliyowasilishwa yatatekelezwa kikamilifu na kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe,Veronika Kessy(aliyesimama) wa tatu kushoto ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Misungwi Bw,Petro Sabato na anayefuata ni Kaimu Mkurugenzi Bw, Benson Mihayo akitoa maelekezo hayo juzi katika kikao cha tathmini na kupokea taarifa ya Maendeleo ya wa shughuli za masoko Wilayani Misungwi
Afisa wa TAKUKURU Wilaya ya Misungwi Bw,Erasto Maonyesho akiwasilisha taarifa ya Uchambuzi wa usimamizi na uendeshaji wa masoko katika kikao cha tathmini ya Maendeleo ya shughuli ya utekelezaji Wilayani Misungwi mapema wiki hii.
Baadhi ya Watumishi na wageni walikwa mbali mbali wakisikiliza kwa makini mjadala wa kikao cha tathmini na maendeleo ya utekelezaji wa shughuli za masoko Wilayani Misungwi, kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri tarehe 9,Januari 2023.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.