Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda apongeza Wananchi wa Kata ya Sumbugu kwa kukamilisha ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa walivyojenga kwa nguvu na michango yao na kuwataka kuhakikisha watoto wao wanasoma kwa bidii na kufuta ufaulu wa daraja sifuri katika mtihani wa kidato cha nne mwaka huu 2020.
Pongezi hizo zimetolewa katika kikao cha Viongozi wa Kata ya Sumbugu na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi wakati wa ziara ya kikazi ya kukagua miradi pamoja na shughuli za maendeleo zinazotekelezwa katika Kata na vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Misugwi, ambapo katika Shule ya Sekondari Sumbugu Madarasa hayo yamejengwa na Wananchi ili kuwezesha kusoma Wanafunzi 247 waliochaguliwa kuanza kidato cha kwanza mwaka huu 2020 katika Shule ya Sekondari Sumbugu.
Mkuu wa Wilaya, Juma Sweda, amesema kwamba Wananchi hao wamejitahidi sana kujenga madarasa kwa nguvu zao na wameonyesha umoja na ushirikiano mkubwa hatimaye wamefanikiwa kujenga vyumba vitano kati ya vyumba saba vinavyotakiwa kulingana na mahitaji ya Wanafunzi 748 wa shule hiyo, ambapo ameahidi kuwachangia kwa kukamilisha ujenzi wa sakafu katika darasa moja.
Akizungumza na Viongozi wa Kata hiyo amewasihi na kuwaeleza umuhimu wa elimu kwa watoto na kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla, na kuwataka kuhakikisha wanaondoa ufaulu wa daraja sifuri katika mtihani wa Kidato cha nne mwaka huu, “ Zero hapana katika Sekondari ya Sumbugu, alisema kwa msisitizo Juma Sweda.”
Amewataka Walimu shuleni hapo kufundisha kwa bidii zaidi na kukamilisha mada zote mapema ili kuwapa fursa wanafunzi kupata mazoezi ya kutosha ya maandalizi ya Mtihani, na amewaonya Wananchi waliozoea na watakaothubutu kuwapa mimba watoto wa shule na kueleza kuwa watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Awali, katika ziara yake Mkuu wa Wilaya huyo amekagua na kuridhishwa na ujenzi wa Nyumba tatu za Walimu zilizojengwa na kukamilika katika Shule ya msingi Sumbugu ambazo pia zimejengwa kwa nguvu na michango ya Wananchi wa Kijiji cha Sumbugu, na kuwaomba Wananchi wa maeneo ya vijiji vingine kuiga mfano huo wa ushirikiano na moyo wa kujituma katika maendeleo kwa lengo la kuboresha na kukuza sekta ya elimu nchini.
Juma Sweda, amewasihi Walimu wa shule hiyo kuwajibika kikamilifu kwa kuzingatia kanuni taratibu na sheria za utumishi wa umma ikiwemo kuwahi kazini na kufundisha kwa bidii na kuwaonya Walimu wenye tabia ya uchelewaji kazini, vitendo ambavyo vinazorotesha maendeleo ya taaluma kwa Wanafunzi na kusababisha kudorola kwa ufaulu katika mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, amekagua na kuona maendeleo katika sekta ya Afya, ambapo katika Zahanati ya Sumbugu amebaini kuwepo kwa utaratibu mbovu wa utunzaji wa kumbukumbu na takwimu za utoaji wa madawa katika stoo ya dawa na kutoa maelekezo kwa TAKUKURU kufuatilia taratibu hizo na kutoa taaarifa mapema.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda (kushoto) akikagua leja ya dawa kuona namna utaratibu wa utoaji dawa katika stoo kwenda kwa Wagonjwa unavyofanywa na utunzaji wa kumbukumbu na akipewa maelezo kuhusu utaraibu kutoka kwa Muuguzi wa Zahanati ya Sumbugu, (katikati ni) Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Sumbugu Ezrom Mwanga akishuhudia zoezi la ukaguzi huo.
Jengo la vyumba vya Madarasa matano vilivyojengwa na Wananchi katika Sekondari ya Kata ya Sumbugu, Madarasa haya yanatarajiwa kuanza kutumiwa na Wanafunzi kuanzia wiki ijayo
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.