Wananchi Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza washauriwa kuzitumia kikamilifu mvua zinazoendelea kunyesha kwa kulima mazao ya chakula na biashara ili kuweza kupata mavuno ya kutosha kwa msimu huu.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda, alipowatembelea baadhi ya Wakulima wa Kijiji cha Nguge Kata ya Mwaniko wakiwemo Wnakikundi cha Jikomboe kwa ajili ya kuhamasisha Wananchi kulima kwa kuzingatia kanuni kumi za Kilimo bora cha pamba..
Juma Sweda amewashauri Wakulima wote Wilayani Misungwi kuzitumia vyema mvua hizi za Vuli kwa kulima mazao ya chakula na biashara ambayo ni Mtama, Mahindi, Viazi, Mpunga, Choroko pamoja na Dengu na Pamba na kuwaomba walime mazao kwa wingi ili yaweze kusaidia kwa Chakula na fedha za matumizi mbalimbali ya familia.
Baadhi ya Wanakikundi cha Jikomboe cha Kijiji cha Nguge wakiendelea na kazi ya Kilimo wakipanda mbegu za pamba kwa mstari kwenye shamba lao la hekari 3 na walitembelewa na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi pamoja na Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ili kuona na kukagua shughuli za kilimo.
Mkuu wa Wilaya huyo pia amepiga marufuku na kukemea Vitendo vya baadhi ya Wananchi kucheza bao na michezo mingine ya Bahati nasibu wakati wa kazi na kilimo na kuonya kwamba atahakikisha watakaojihusisha na michezo hiyo sheria zitachukuliwa dhidi yake pamoja na kupewa kazi ya kufanya mashambani.
Kwa upande wake Afisa Kilimo, Ushirika na Umwagiliaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Majid Kabyemela awali alisema kuwa katika Wilaya ya Misungwi katika msimu huu inatarajia kulima hekta 15,040 za kilimo cha zao la Pamba, ambapo tayari Maafisa ugani wameshatoa elimu na hamasa kwa Wakulima ya kulima kwa kuzingatia kanuni10 za kilimo bora cha pamba ikiwa ni pamoja na kupanda kwa mstari, matumizi ya mbolea ya samadi na virutubisho, kupunguza miche shambani, kupanda mapema, kunyunyuzia dawa kuzuia wadudu, na kuvuna mapema na kuchambua pamba vizuri.
Afisa Kilimo na ushirika huyo alieleza kwamba maandalizi ya msimu huu yamekamilika na mbegu za pamba aina ya UK 08 ziligawiwa kwa Wakulima mapema na wengi wao wamehapanda kwa wakati na Wataalam wa Kilimo wanaendelea na zoezi la kufuatailia na kuwashauri Wakulima hao.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda (aliyeinama chini kulia) akipanda mbegu za pamba katika shamba la hekari 3 la Kikundi cha Jikomboe Kijiji cha Nguge ( kushoto) ni Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi Petro Sabatto wakionyesha mfano wa kilimo bora cha pamba kwa kupanda kwa mstari.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.