Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Paulo Chacha amewagiza Viongozi wa Tarafa, Kata na Vijiji kuwasaka na kuwakamata Wazazi ambao hawajawapeleka watoto kuripoti shule kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka 2023 Wilayani Misungwi.
Mhe, Paulo Chacha ametoa agizo hilo mapema leo katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Misungwi mara baada ya kubaini na kuona hali halisi ya watoto ambao wamesharipoti na kuanza masomo ya Kidato cha kwanza tangu tarehe 8, Januari 2024 na kutoridhishwa na mahudhurio ya Wanafunzi wa Kidato cha kwanza.
Amewataka Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Vijiji kwa kushirikiana na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji kuwabaini Wazazi na Walezi wa watoto wote ambao mpaka sasa hawajaanza masomo na kuwapeleka Kituo cha Polisi kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kisheria kwa kosa la kuwanyima watoto haki ya msingi ya kupata elimu ya Sekondari ambapo amekea suala la Wazazi kiuwaozesha watoto na wengine kuwapeleka kufanya kazi za kilimo na mifugo pamoja na uchimbaji wa madini.
Aidha, agizo hilo pia linahusu Wazazi wenye watoto ambao hawakufanya Mtihani wa Kidato cha pili Wanafunzi wapatao 630 kutoka katika shule zote 37 za Wilaya ya Misungwi pamoja na wanafunzi wa Kidato cha Nne mwaka 2023 wote kwa pamoja watafutwe na kurejeshwa shule kwa ajili ya kuendelea na masomo na kufanya mitihani husika.
Mkuu wa Wilaya huyo ameipongeza rasimu ya Bajeti ya Halmashauri na kuwataka Watendaji kujipanga vizuri kutekeleza miradi kwa uadilifu na kuikamilisha kwa wakati na ubora na kwa viwango pamoja na kuweka jitihada kubwa katika ukusanyaji wa mapato ya ndani na kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuleta tija katika jamii.
Awali akiwasilisha rasimu ya Bajeti katika kikao hicho cha kupitia mapendekezo ya rasimu ya Bajeti ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bi. Peniel Titus amesema kuwa Halmashauri inatarajia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi Bilioni 51.4 kwa ajili ya utekelezaji wa wa shughuli mbalimbali za Halmashauri ikwa ni pamoja na malipo ya Mishahara ya Watumishi kiasi cha shilingi Bilioni 36,792,448,000, fedha za Ruzuku ya uendeshaji wa Ofisi (OC) kiasi cha shilingi 1,359,841,000, na katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa shilingi Bilioni 8,636,386,000.
Afisa Mipango huyo alieleza kwamba kwa upande wa na Mapato ya ndani Halmashauri imekisia kukusanya na kutumia kiasi cha shilingi 4,677,820,361 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani ambapo kati ya fedha hizo Bilioni 3,946,152,361 ni Mapato halisi na Shilingi Milioni 31,668,000 ni Mapato Lindwa.
Bi. Peniel Titus ameongeza na kufafanua kwamba makadirio ya Mapato ya ndani kwa Mwaka 2024/202425 yameongezeka kwa asilimia 4.15 kutoka Shilingi Bilioni 4,483,664,000.04 mwaka 2023/24 hadi shilingi Bilioni 4,677,820,361.3 kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa matumizi ya mfumo wa kielektoniki wa ukusanyaji wa mapato ikiwa na kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinawekwa Benki kwa wakati, kuongezeka kwa watumiaji wa madini ujenzi hususani mchanga na mawe iliyopelekea kuongezeka kwa mapato ya madini ya ujenzi pamoja na kuongezeka kwa idadi ya viwanda na makampuni yaliyopelekea kupanda kwa ushuru wa huduma.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Maji safi na taka Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Misungwi Mhandisi Bw. Marwa Kisibo ameeleza kuwa kiasi cha fedha kilichotengwa katika Bajeti 2023/2024 ni Shilingi Bilioni 1,986,416,209.67 kitanufaisha zaidi ya wakazi 173,031 katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi ambapo baadhi ya hiyo ni Mradi ya Mabuki,Ilujamate –Buhingo,Kigongo,Ukiliguru,Koromije hadi Usagara,Igongwa,Nguge,Mabale Mbarika,Kijima hadi Isakamawe,Ngaya- Matale.
Sambamba na hayo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili Miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya Wananchi na kuahidi kusimamia kikamilifu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ili miradi hiyo iweze kuleta tija kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Naye Katibu wa CCM Wilaya ya Misungwi Bw. Mwita Nyarukururu ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa ushirikiano mzuri na kusimamia kikamilifu pamoja na juhudi zinazofanyika kuhakikisha Mapato ya ndani yanaongezeka,na kuwataka Watendaji kuendelea kusimamia ukusanyaji wa mapato vizuri pamoja na mchakato wa kuwa na POS katika ngazi za Vijiji ili kuokoa mapato yanayopotea katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi na kwamba CCM itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
Mkuregenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Bw,Joseph Mafuru aliyesimama kwa mbali akitoa ufafanuzi kwa wajumbe juu ya mapendekezo ya mpango wa Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa fedha 2024/2025 katika Ukumbi wa Halmashauri ya Misungwi.
Katibu wa CCM Wilaya ya Misungwi Bw, Mwita Nyarukururu kushoto akizungumza katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya kilichofanyika katika ukumbi wa Halmashauri kwa ajili ya kupitia Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Halmashauri ya Mwaka 2024/2025.wa pili kushoto ni Katibu Tawala Wilaya Bw, Abdi Makange akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe,Paul Chacha (kulia) pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Misungwi Bw,Joseph Mafuru wa kwanza (kulia).
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.