Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi yatoa Tuzo na Zawadi kwa Walimu mahiri 49 wa Shule za msingi na Sekondari waliofanya vizuri katika Shindano lililoandaliwa kwa lengo la kutoa motisha kwa Walimu Mkoani Mwanza.
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Misungwi, lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe, Veronika Kessy amesema kwamba kuna umuhimu kwa Walimu kupata motisho kutokana na utendaji kazi mzuri wenye kuleta tija katika Sekta ya Elimu.
Bi, Veronika Kessy ametoa pongezi za dhati kwa Shirika hilo lisilo la Kiserikali kwa kujitokeza katika kufadhali baadhi ya Shule za Msingi na Sekondari katika Kata za Idetemya na Mwaniko kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwemo kukarabati vyumba vya madarasa,matundu ya vyoo na kujenga vyumba vya madarasa katika shule hizo.
Kwa upande wake Mratibu wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la Africa School Assistance Project Bw, Jackson Mzenya ameeleza kuwa shirika hilo linafanya kazi katika Mikoa miwili Arusha na Mwanza,ambapo kwa Mwanza wamejikita katika Wilaya ya Misungwi pamoja na jamii zake na kufanikiwa kufanya kazi katika shule 8 kuanzia 2014 hadi 2022,ambapo lengo la shirika ni kutanua wigo wa kutoa huduma kusimamia na kuboresha shule ambazo ziko nje ya miji zinapata Elimu bora na wanafunzi kutimiza ndoto zao.
Bw, Mzemya alifafanua kuwa Tuzo hizo za Walimu zimetolewa baada ya kufanya shindano lililoshirikisha Shirika la Africa School Assistance Project pamoja na Shirika la The Foundation For Tomorrow ambapo wameweza kupata Walimu 49 miongoni mwao Walimu 35 kutoka Shule za msingi na Sekondari wamepata Zawadi ya vyeti na fedha shilingi 500,000/= kila mmoja kwa jumla ya shilingi 17,500,000/= na Walimu 14 wamepatiwa vyeti pekee ikiwa ni motisha na kuwaongezea chachu katika uwajibikaji katika kufundisha Wanafunzi.
Wakati huo huo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mhe, Kashinje Machibya kwa niaba ya Barazala Madiwani la Halmashauri amesema na kuwasihi Walimu wote kuendelea na moyo na kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha na kuwa waadilifu na wasithubutu kuchezea fedha za umma ambazo zinatolewa na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali katika sekta ya elimu.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Misungwi Bw. Benson Mihayo ameshukuru Shirika hilo kwa kuendelea kufadhili baadhi ya shule za Elimu ya Msingi na Sekondari na kuwaomba waende mbali zaidi katika shule ambazo ziko pembezoni mwa Wilaya ya Misungwi kutoa huduma bora ambapo itapelekea chachu ya maendeleo ya Elimu katika Shule hizo.
Bw. Benson Mihayo amesisitiza kupitia shirika hilo wamejipanga kimkakati kuhakikisha wanashirikiana bega kwa bega kuinua Elimu katika Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa kuwapongeza Walimu kwa kutoa zawadi na vyeti kwa wale ambao wafanya vizuri zaidi kwa lengo la kwa motisha kuendelea kutoa huduma iliyo bora katika vituo vyao vya kazi.
Mmoja wa Walimu waliopata Zawadi ya Cheti na Fedha taslimu shilingi 500,000/= Bw, Leonald Maige kutoka shule ya msingi Misungwi, amesema kwamba amepata faraja na Amani baada ya kupata Zawadi ya Cheti na fedha shilingi 500,000/= na kueleza kuwa Walimu ni wito na kujituma kwa bidii ambapo amewashauri Walimu wengine kipindi kijacho watumie fursa hii n akushiriki katika shindano la kupata Walimu mahiri na bora kwa lengo la kupata motisha na kuongeza ari na moyo wa kufanya kazi ya kufundisha kwa manufaa ya Halmashauri na taifa kwa ujumla.
Mkuu wa Wilaya ya Misungwi katikati Mhe,Veronika Kessy akiwa na viongozi mbalimbali waliohudhuria katika hafla fupi ya kuwapongeza walimu mahiri katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Misungwi siku ya Ijumaa.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.