Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi,Mkoani Mwanza limepitisha Makisio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020 ya kukusanya na kutumia shillingi Billioni 56.5 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya maendeleo, Mishahara ya Watumishi pamoja na matumizi ya kawaida .
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mhe Antony Bahebe Masele alieleza haya katika Mkutano wa Baraza maalum la Madiwani lililofanyika katika Ukumbi wa MGS Mjini Misungwi hivi karibuni, kwa ajili ya kujadili na kupitisha makisio ya Bajeti ya mapato na matumizi ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 ambapo Halmashauri imeweka makisio ya kukusanya kiasi cha fedha Billioni 56,5 zitokanazo na Mapato ya Ndani ya Halmashauri, na ruzuku toka Serikalini.
Akiwasilisha taarifa ya Makisio ya Bajeti hiyo , Afisa Mipango wa Halmashauri , Bi Anna Urioh kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri alisema kwamba katika mwaka wa fedha 2019/2020 Halmashauri ya Misungwi imepanga kukusanya na kutumia Bajeti ya fedha yenye jumla ya shillingi Billioni 56,516,376,608/= ambapo kati ya fedha hizo, shilingi 2,830,722,000/= zitatokana na Mapato ya ndani ya Halmashauri , shillingi 37,830,717,000/= ni fedha kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi ,shillingi 14,838,549,323/= ni bajeti ya fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo pamoja na shillingi 1,047,110,285 /= ni fedha za ruzuku ya Serikali kwa ajili ya matumizi ya kawaida .
Afisa Mipango wa Halmashauri Bi, Anna Urioh akiwasilisha Makisio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020 katika Baraza la Madiwani kwa ajili ya kupitisha na kubariki
Bi,Anna Urioh alifafanua kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi katika Bajeti ya mapato ya ndani kwa mwaka 2019/2020 ya shillingi 2,830,722,000/= imekuwa na ongezeko la makadirio ya kukusanya Mapato ya shilling 421,951,000/= ukilinganisha na makisio ya Bajeti ya mapato ya ndani ya mwaka 2018/2019 ambayo yalikuwa ni shillingi 2,408,771,000/= ambapo hadi kufikia mwezi Disemba 2018 Halmashauri ilikuwa imekusanya jumla ya shillingi 824,133,778/= sawa na asilimia 34% ya makusanyo ya Mapato yote.
Mkurugenzi Mtendaji Wilaya Bw, Kisena Mabuba akizungumza jambo katika majadiliano ya Makisio ya Bajeti ya mwaka 2019/2020 katika Mkutano wa Baraza la Madiwani.
Afisa Mipango huyo aliongeza kwamba ongezeko la bajeti ya mapato ya ndani katika Bajeti ya mwaka 2019/2020 limetokana na kuzingatia mapendekezo ya Kamati mbalimbali za Halmashauri pamoja na Menejimenti kubuni vyanzo vipya na kuwa na takwimu nzuri na halisi ya Wafanyabiashara wa aina mbalimbali ikiwemo Machinjio, Minada , Standi, Madini, na mengine .
Mhe, Antony Bahebe Masele alisema kuwa Baraza la Madiwani la Halmashauri hiyo limejipanga kikamilifu katika kusimamia na kufuatilia kwa makini utekelezaji wa Bajeti iliyopitishwa, hususani katika suala la ukusanyaji wa Mapato ya ndani ambayo yameongezeka katika bajeti ya mwaka ujao na Madiwani watahakikisha wanashirikiana kwa dhati na Watendaji wote ili kuweza kufika malengo ya kukusanya mapato hayo na kueleza kuwa vyanzo vipo vingi cha muhimu ni uwajibikaji na usimamizi mzuri.
Alisisitiza na kueleza kwamba Baraza la Halmashauri hiyo litawachukulia hatua za Kinidhamu Watendaji wote watakaoshindwa ama kuzembea katika jukumu la ukusanyaji wa Mapato na Madiwani watahakikisha wanafuatilia chanzo kimoja kimoja na kuwaomba Watendaji kuwajibika ipasavyo na kuhakikisha vyanzo vyote vinakusanywa kwa asilimia zote na kufikia malengo.
Baadhi ya Madiwani wakifuatilia mjadala na maoni ya Makisio ya Bajeti katika Mkutano wa Baraza la Madiwani la Bajeti
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo,Bw,Kisena Mabuba alisema kwamba Menejimenti ya Halmashauri katika maandalizi ya bajeti ya mwaka 2019/2020 imezingatia maelekezo mbalimbali ya Serikali ya wamu ya tano ya kisekta pamoja na malengo ya Wilaya na Vipaumbele vya kiwilaya ambavyo vinalenga kujibu matarajio ya Serikali ya awamu ya tano, na kulingana na Mwongozo wa bajeti uliotolewa.
Bw, Kisena Mabuba amewataka Madiwani pamoja na Watendaji wa Halmashauri kuhakikisha wanatekeleza shughuli zaa Halmashauri pamoja na miradi ya Maendeleo kwa kuzingatia na kufuata Bajeti kama ilivyopitishwa na kuidhinishwa na Serikali na kuhakikisha Ukusanyaji wa Mapato ya ndani unafikia malengo kupitia vyanzo vyote vilivyoanishwa.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.