Baraza la Madiwani laridhia matumizi ya shilingi Bilioni 1.4 sawa na asilimia 70.47% zilizotekeleza miradi ya maendeleo katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024/2025 katika Halmashauri ya Wilayani Misungwi, Mkoani Mwanza.
Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Madiwani uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri tarehe 29 Oktoba 2024, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi Mhe, Kashinje Machibya amesema shilingi Bilioni 1.4 zimetumika katika kuwaletea wananchi maendeleo ikiwa ni pamoja na kuongeza na kuboresha miundombinu ya huduma za kijamii kama vile huduma za Sekta ya kilimo, Maji Barabara na Madaraja, Vituo vya Afya na Zahanati na Sekta ya Elimu
Mhe, Machibya amesema kuwa miradi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya wilaya na yanatarajiwa kuboresha maisha ya wananchi ambapo uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha hizo utahakikisha kwamba kila shilingi inatumika kwa manufaa ya jamii ikiwa ni pamoja na kuwapa huduma stahiki katika kutatua kero mbalimbali zinazotokea katika sekta hizo na kuhakikisha wanaondokana nazo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Misungwi Bw. Addo Missama amesema Watendaji wa Serikali wanapaswa kuendelea na utendaji kazi wa maendeleo ambapo matumizi bora ya fedha hizo katika miradi ya maendeleo yanayohusu elimu, afya, na miundombinu ni muhimu kuhakikisha kwamba fedha hizo zinatumika kwa ufanisi ili kuboresha maisha ya wananchi wa Misungwi na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wao Wajumbe wa Baraza hilo walipongeza hatua hiyo na kutoa mapendekezo mbalimbali ya kuboresha usimamizi wa miradi na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Wananchi katika kutekeleza miradi hiyo ili kuhakisha fedha zinatumika ipasavyo na kufikia malengo yaliyokusudiwa hivyo walikubaliana kuimarisha ushirikiano kati ya ofisi za Serikali na jamii ili kufanikisha malengo ya maendeleo ya Wilaya.
Mkutano huo wa Baraza la madiwani ulihudhuriwa na Viongozi wa Serikali pamoja na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi, Wataalamu kutoka katika Idara na Vitengo mbalimbali vya Halmashauri ya Misungwi pamoja na Wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.