Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Mkoani Mwanza laridhia na kupitisha rasimu ya Bajeti ya mapato na matumizi ya shilingi Bilioni 44.3 kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
Akizungumza katika Mkutano maalum wa Baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kashinje Erasto Machibya amesema kwamba Halmashauri ya Misungwi imepanga kukusanya na kutumia jumla shilingi Bilioni 44.3 katika mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo fedha hizo ni kutokana na vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri yenye jumla ya shilingi Bilioni 2. 4 pamoja na fedha za ruzuku toka Serikali kuu shilingi Biliioni 41.8.
Mhe, Kashinje amesema katika Bajeti hiyo Baraza limeridhia mpango wa ujenzi wa Kituo cha Afya kwa gharama ya shilingi milioni 400 fedha ambayo inatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri pamoja na kuendelea kukamilisha miradi mingine katika sekta ya Afya, Elimu, Maji, Umeme, Mazingira na mingineyo.
Amewataka Madiwani kuwa na utamaduni wa kusimamia miradi ya maendeleo vizuri inayotekelezwa katika maeneo yao na kwamba wanapaswa kufahamu fedha zote zinazotolewa na Serikali pamoja na michango ya wadau na nguvu ya Wananchi yote isimamiwe kikamilifu na miradi itekelezwe kwa kiwango na ubora.
Akiwasilisha rasimu hiyo ya Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka 2021/2022, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Kaimu Afisa Mipango Mwanajumbe Zuberi amesema katika mwaka wa Fedha 2021/2022 Halmashauri imetenga jumla ya shilingi Bilioni 44,324,862,080. na kati ya hizo shilingi Bilioni 2,498,951,580. zitatokana na Mapato ya Ndani (Own source) na shilingi Bilioni 41,825,910,500. ni fedha kutoka serikali kuu na kati ya fedha yote inayotoka serikali kuu shilingi, Bilioni 35,498,052,000. ni kwa ajili ya kulipa mishahara ya watumishi wa Halmashauri, ambayo ni sawa na asilimia 84.87 ya Bajeti yote inayotoka Serikalini.
Alieleza kwamba katika bajeti hiyo jumla ya shilingi Bilioni 1,443,559,000. ni Ruzuku kutoka Serikali kuu kwa ajili ya matumizi ya kawaida (OC), shilingi Bilioni 4,884,299,500. ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo, na shilingi Bilioni 35,498,052,000. ni kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi pia Halmashauri imetenga jumla ya shilingi Milioni. 713,608,632. kutoka katika Mapato ya Ndani kwa ajili ya kutekeleza shughuli za Maendeleo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi, Kisena Mabuba amesema makisio ya Bajeti hiyo yamelenga kuwaletea maendeleo Wananchi wa Wilaya ya Misungwi kutokana na kubuni vyanzo vya mapato vipya ikiwa ni pamoja na kutenga fedha za fidia ya ardhi kwa ajili ya kutwaa maeneo kikiwemo Kisiwa cha Buzumo Kata ya Mbarika ambacho matarajio ya kuwekeza kuwa eneo la utalii kwa kuweka Wanyama wasio wakali na kuimarisha utalii na kuwa chanzo cha mapato ya Halmashauri.
Bw, Kisena Mabuba ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi imeweka mipango na mikakati ya kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa viwango na suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani unafanyika kwa uadilifu na uaminifu na fedha yote inaelekezwa katika maeneo yaliyopangwa na kukusudiwa na hakutokuwepo kwa ubadhilifu wowote.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya ya Misungwi, Petro Sabatto ambaye alimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda amesema kwamba amepongeza juhudi zilizofanywa na Wataalam na kundaa Bajeti nzuri na kuwataka Madiwani kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao na kuhakikisha inakuwa ya viwango na thamani ya fedha inaonekana.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.