Waziri wa Fedha Mhe, Mwingulu Nchemba awahakikishia Wananchi wa Wilaya ya Misungwi kuwa Serikali itaendelea kukamilisha utekelezaji wa Miradi ya maji ya Ukiriguru na mingine ambayo imesuasua kutokana na changamoto za fedha na Wizara imeshachukua hatua za malipo ya miradi husika Wilayani Misungwi.
Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameyabainisha hayo tarehe 15 Septemba, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya Taasisi ya Chuo cha Uhasibu Tanzania Kampasi ya Mwanza (TIA), iliyojengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi Bilioni 7.8, kitakachokuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi zaidi ya 5,000 kwa wakati mmoja, na kuahidi kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewekeza rasilimali fedha katika sekta mbalimbali za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu pamoja sekta ya maji na miumdombinu ya barabara na kuwataka Wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Rais Samia ambapo Wizara ya fedha tayari imeshaandaa malipo ya Mkandarasi wa mradi wa Maji wa Ukirigurtru hadi Usagara na Serikali itaendelea kutoa fedha kwa awamu ili kukamilisha miradi hiyo.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Alexander Mnyeti, amezungumzia changamoto zinazokabili miradi ya maji katika jimbo la Misungwi amesema kuwa Mkandarasi anasuasua sana wa mradi wa Maji wa vijiji 16 kutoka chanzo cha maji cha Ihelele ameomba Wizara itatue na kuweka Mkandarasi mwingine ili utekelezaji ukamilike kwa haraka pamoja na kusuasua kwa mradi wa maji wa Ukiriguru hadi Usagara unaotekelezwa polepole sana kwa sababu Mkandarasi hajalipwa fedha kitendo ambacho kinasababisha kusuasua kwa mradi huo na kumsisitiza Waziri Nchemba aweze kushughulikia na kuhakikisha Wakandarasi wanalipwa kwa wakati na miradi ikamilike na hatimaye kukidhi matarajio ya Wananchi wa Misungwi.
Mhe. Mnyeti ameongeza kwamba sambamba na miradi ya maji pia ameomba kulipwa kwa Mkandarasi wa barabara ya Mwanangwa – Misasi hadi Kahama ambaye amesimama kutokana na madai ya fedha ili kuendelea na kazi katika barabara hiyo muhimu kwa uchumi na huduma za kijamii pamoja na kuongeza Vifaa tiba vya thamani ya shilingi milioni 500 katika Hospitali ya Wilaya ya Misungwi ili Wananchi wapate huduma bora ya kisasa.
Mhe, Nchemba ameipokea changamoto ya Miradi ya maji kuhusu kususua kwa Wakandarasi na kuweka wazi kwamba Wizara ya fedha itahakikisha inakamilisha malipo na hundi ipo tayari kwa ajili ya kumlipa Mkandarasi huyo wa mradi wa Maji wa Ukiriguru hadi Usagara ambaye hajalipwa malipo hayo ambayo yataongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo wa maji ambao umelenga kuwakomboa na kuboresha maisha ya Wananchi wa Usagara na Wilaya ya Misungwi.
Akitoa salamu za Wilaya kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi Mhe. Johari Samizi, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita, inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuipatia Wilaya yake, zaidi ya shilingi Bilioni 39 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika Wilaya hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ambazo zimeelekezwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo sekta za afya, elimu na maji.
Halmashauri ya Wilaya Misungwi
Sanduku la Posta: P.O Box 20 MISUNGWI
Simu ya Mezani: +255282983268
Simu ya Mkononi: 0717259106
Barua Pepe: ded@misungwidc.go.tz
Copyright ©2021 Misungwi District Council . All rights reserved.